HABARI MPYA LEO  

JAJI MUNUO (TZ) ATEULIWA KUWA RAIS WA CHAMA CHA MAJAJI WANAWAKE DUNIANI

By Maganga Media - May 10, 2012

JAJI wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Jaji Eusebia Munuo ameteuliwa kuwa Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani, imebainika. Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam jana Munuo alisema kuwa uteuzi huo umefanyika mnamo tarehe 06.Mei mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa Majaji Wanawake Duniani uliofanyika nchini Uingereza hivi karibuni.


“Nafasi hii ya Urais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) nimeipata kufuatia aliyekuwa Rais wa Chama hiki kutoka Uingereza kumaliza muda wake, na tumekabidhiwa rasmi bendera ya Chama katika mkutano uliofanyika hivi karibuni nchini Uingereza,”alisema Jaji Munuo.

Aliongeza kuwa nafasi hii ataishikilia mpaka tarehe 9. Mei ya mwaka 2014 ambapo uchaguzi mwingine utafanyika na kumpata Rais kutoka nchi nyingine.

Hata hivyo alibainisha kuwa mkutano mwingine wa Chama hiki unatarajiwa kufanyika nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha mnamo kuanzia Mei 6-9 mwaka 2014 ambapo kiti hiki cha urais kitakabidhiwa kwa nchi nyingine.

Jaji Munuo ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendeleza na kupigania maslahi ya Majaji Wanawake na wanawake duniani.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Engella Kileo alibainisha kuwa uteuzi wa Mhe. Munuo umeleta faraja hasa kwa Majaji na Mahakimu wa nchi hii na hivyo kuahidi kushirikiana nae katika kufanikisha upatikanaji wa haki kwa usawa.


“Uteuzi wa Mhe. Munuo umefuatiwa na utendaji kazi wake pamoja na ushiriki wake ulio imara katika mikutano hii ambayo hufanyika nchi mbalimbali na hatimaye kupelekea wasifu wake kufahamika kwa wanachambalimbali wa chama hicho,” alisema Jaji Kileo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT).

Jaji Munuo alianza kazi rasmi mwaka 1970 kama Hakimu Mkazi wa kwanza mwanamke, na hivi sasa ni mmoja kati ya Majaji watano wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.


Na Mary Gwera-Mahakama ya Rufani (T)

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII