HABARI MPYA LEO  

KAMATI KUU YA CCM YARIDHIA BARAZA LA MAWAZIRI KUVUNJWA

By Maganga Media - Apr 27, 2012

Nape akizungumza na waandishi jioni hii.

Kamati Kuu iliyokutana leo tarehe 27/04/2012  chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Jijini Dar es salaam, pamoja na mambo mengine imefanya maamuzi kadhaa ikiwemo kumridhia Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri.

 
Ifuatayo ni taarifa Kamili kama ilivyosomwa kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye.

Rais amepokea taarifa na maazimio ya Kamati ya wabunge wa CCM na Kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM juu ya kilichotokea kwenye bunge lililopita mjini Dodoma.

Taarifa hizo zimewasilishwa kwenye kamati kuu na kujadiliwa. Pamoja na taarifa hizo kamati Kuu imepokea taarifa ya jinsi Rais alivyojipanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na watendaji wa serikali na wale wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioinishwa na  taarifa ya Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali, Kamati za kudumu za bunge na wabunge bungeni.

Kamati Kuu imeamua yafuatayo;
1. Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa serikali yao.Inapongeza juhudi za serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa.

2.Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais   KULISUKA UPYA BARAZA LA MAWAZIRI na taasisi zingine zilizoanishwa katika ripoti hizo. Imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo ufanywe mapema iwezekanavyo.


Aidha kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya baraza la wawakilishi Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa taarifa yao.

Kamati Kuu inawapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa jinsi walivyojadili taarifa hiyo na pia Kamati Kuu inaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa na kuanza kuifanyia kazi.

A. UTEUZI
Kamati Kuu imeteua wafuatao kuwa makaimu Katibu wa mikoa. Vituo vyao vya kazi vitapangwa baadae. Uteuzi huu unatokana na kuwepo kwa mikoa wazi mitano, mikoa hiyo ni;

Geita,Njombe,Simiyu,Katavi,Magharibi.

Hivyo wafuatao wameteuliwa kuwa makaimu Katibu wa CCM wa Mikoa.

1. Ndg. Hilda Kapaya

2. Ndg. Shaibu Akwilombe

3. Ndg. Hosea Mpangile

4. Ndg. Alphonce Kinamhala
 
5. Ndg. Aziz Ramadhani Mapuri


Imetolewa na
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi.





Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII