ASKOFU APINGA UZAZI WA MPANGO
By Maganga Media - Apr 27, 2012
HUKU serikali ikiendeleza mikakati ya kutoa elimu juu ya uzazi wa Mpango, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dk. Moses Kulola amepingana na sera hiyo na kusema ni kuingilia maamuzi ya Mungu.
Kiongozi huyo alisema kuwa hakuna sababu yoyote ya serikali kuweka mikakati ya kutoa elimu ya kufunga kizazi kwani hiyo ni kazi ya Mungu mwenyewe. Alisema kuwa kuna kila sababu ya kuikemea mipango hiyo kwani suala la kudai kuwa pawepo na uzazi wa mpango ni kuwa na hofu ambayo inasababishwa na shetani, jambo ambalo ni hatari kwa taifa.
“Mimi nilifyatua watoto kumi na sikushindwa kuwasomesha japo wapo watu ambao walikuwa wakisema kuwa watanishinda kuwasomesha,” alisisitiza Dk. Kulola.
Kwa upande mwingine, kiongozi huyo mkuu wa Kanisa la EAGT aliwakemea watumishi wa serikali ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi. Askofu Dk. Kulola alisema kuwa anasikitishwa na baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakijivunia vyeti vyao ambavyo vinaonyesha elimu walizonazo lakini wanashindwa kutimiza wajibu wao pindi wawapo ofisini.
Kiongozi huyo alisema kuwa wapo baadhi ya wasomi ambao wanachukua masomo yao kutoka nchi za nje lakini cha kushangaza pindi wanaporudi nchini wanashindwa kufanya kazi zao kama inavyostahili.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, amewataka wasomi wa vyuo vikuu nchini kuwa mfano katika jamii tofauti na ilivyo sasa.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII