HABARI MPYA LEO  

WANAFUNZI WA KIKE WAKERWA KUFANYISHWA BIASHARA!

By Maganga Media - Feb 21, 2012

WANAFUNZI wa kike wa shule za msingi mbalimbali wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga wameiomba Serikali iingilie kati iwazuie wazazi wao kuwafanyisha biashara ndogondogo barabarani ili kupunguza mimba za utotoni.

Katika mdahalo wa utetezi wa haki za wanafunzi uliofanyika juzi, wanafunzi wa shule 18 zilizopo katika kata za Lunguya , Bugarama, Bulyanhulu na Mwingiro walisema pamoja na kufanyishwa biashara usiku kando ya barabara itokayo Kahama kwenda mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, pia hulazimika kuzungusha bidhaa kwenye baa.

Katika mdahalo huo uliofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Care International tawi la Kahama, wanafunzi hao walisema kuwa wazazi wamekuwa wakiwapa bidhaa kama vile mahindi, karanga, vitumbua na kutembeza pembezoni mwa barabara hiyo nyakati za usiku hali ambayo inaweza kuchangia kuingia katika vishawishi.

Mmoja wa wanafunzi hao kutoka katika Shule ya Msingi ya Lunguya, Mariamu Pamba alisema wamekuwa katika wakati mgumu kwani kwa kufanya hivyo wanapoteza muda wao wa kusoma nyakati za usiku.

“Tunaomba Serikali iingilie kati suala hili kwani kwa kuwaruhusu wanafunzi kufanya biashara nyakati za usiku kunaweza kuchochea kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji katika kata hii,” alisema Mariamu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lunguya, Benedicto Manwari alisema kuwa tatizo hilo limeshafikishwa ofisini kwake na linafanyiwa kazi na uongozi wa kata hiyo na kazi ya utekelezaji kuhakikisha tatizo hilo linaisha.

Manwari alisema kitendo cha wanafunzi kutembea usiku ni kibaya. Alisema wazazi wanatakiwa kuwaacha wanafunzi hao kujisomea na kujijengea misingi mizuri ya maisha yao ya baadaye.

Mratibu wa Mdahalo huo kutoka katika Shirika la Care International Tawi la Kahama, Rehema Mwakajala alisema mradi wake wa miaka mitatu wa kuwawezesha watoto wa kike kupitia michezo, unaisha mwezi ujao.

Mwakajala alisema kuwa jumla ya Wanafunzi wa kike karibu 17, 870 wamekwishapata mafunzo juu ya stadi za uongozi .
Na habari leo

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII