HABARI MPYA LEO  

UDANGANYIFU WA MITIHANI HATARI KWA TAIFA

By Maganga Media - Feb 21, 2012


HIVI karibuni serikali imewasamehe wanafunzi 9,629 wa darasa la saba mwaka jana waliofutiwa matokeo ya mtihani kutokana na udanganyifu.
Madai ya serikali kuhusu kutolewa kwa msamaha huo ni kwamba idadi ya wanafunzi hao ni kubwa na kwamba hali hiyo itawahusu wanafunzi waliogundulika kuwa na majibu yaliyofanana tu na sio 107 waliofutiwa matokeo yao baada ya kukutwa na majibu.
Hatua hiyo ya serikali ambayo ilitangazwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Malugo kwa namna moja ni kama inafanana na hatua iliyochukuliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Oktoba 6, 2008 lilipotangaza kuwa limefuta mtihani wa somo la hisabati wa taifa kwa kidato cha nne uliokuwa ufanyike siku hiyo baada kugundulika kuwa ulikuwa umevuja.
Katibu Mtendaji wa NECTA Dk. Joyce Ndalichako alisema jijini Dar es Salaam kuwa taasisi anayoongoza ilifanya uchunguzi wa kina na kuridhika kwamba mtihani huo ulivuja. NECTA
ilitangaza kuwa ingetunga mtihani mwingine ambao ungefanyika Jumatatu iliyofuata, Oktoba 27.
Uchunguzi wa waandishi wa habari ulitoa matokeo kuwa mtihani huo ulikuwa umevuja nchi nzima na ulikuwa ukiuzwa mitaani kati ya sh 80,000 na sh 300,000 kila nakala.
Miezi minne iliyotangulia NECTA ilitangaza matokeo ya mitihani ya vyuo vya elimu na kusitisha kutoa matokeo ya watahiniwa 1,066 wa Chuo cha Ualimu cha Kange, mkoani Tanga.
Dk. Ndalichako alisema kulikuwa na taarifa za udanganyifu wakati mitihani hiyo ikifanyika Mei mwaka huu.
Akifafanua, Joyce Ndalichako alisema wanafunzi 405 wa chuo hicho waliofanya mtihani wa ualimu wa daraja ‘A’ picha zao hazifanani na zile walizopigwa wakati wakifanya mitihani hiyo.
Alisema pia kuwa NECTA ilikuwa imefuta na kusitisha matokeo ya wanafunzi mbalimbali kwa sababu tofauti kutokana na kutolipa ada za mitihani na wengine kuhusika kufanya udanganyifu wakati wa kufanya mitihani yao ya taifa.
Vyuo 11 vya ualimu nchini viliwasajili wanafunzi kujiunga na mafunzo ya ualimu kinyume na taratibu, kwa vile walimaliza masomo ya elimu ya sekondari Oktoba 2006, ilhali mafunzo waliyosajiliwa yalikuwa yameanza Julai 20 wakati matokeo ya CSEE yalitangazwa Februari 2007.
Alibainisha kuwa udanganyifu mwingine ulitokea katika Chuo cha Ualimu Tarime ambako watahiniwa wenye namba E0529/0380 na E0529/0380 waliongezwa na wasimamizi vituoni wakati wa mitihani bila idhini ya NECTA.
Kauli kali ya Dk. Ndalichako inasema: “Tumegundua udanganyifu mkubwa katika matokeo ya mitihani iliyofanyika Mei. Baadhi ya watu waliohusika na udanganyifu huo tumewapa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutaka kufanya udanganyifu.”
Kimsingi kilichotajwa hapo juu ni kutamalaki kwa wizi na udanganyifu kwenye suala la mitihani kama sio kwenye sekta ya elimu na hivyo kusababisha ionekane kuwa na dosari za wazi zilizo na mustakabali mbaya kwa taifa.
Hizo ni habari mbaya lakini sio habari za ajabu kwani wizi wa mitihani na udanganyifu ni jambo kongwe na sugu hapa nchini.
Hapa zinaweza kufanyika rejea kadhaa kwa miaka iliyopita ambapo mwaka 1998 uvujaji wa mitihani ya kidato cha nne ulikuwa mkubwa hadi NECTA ikalazimika kufuta mitihani yote nchi nzima na baadaye kufanyika upya mapema mwaka 1999.
Lakini jambo baya zaidi ni kwamba kwa njia hizo za wizi hoja inayoibuka ni kuwa wataalamu tutakaokuwa nao na hata tulionao hivi sasa lazima watakuwa na walakini katika utendaji wao.
Hivi sasa Tanzania ina viongozi na wataalamu wa aina mbalimbali katika sekta zote za uchumi na huduma za kijamii ambao elimu yao inaweza kuelezwa kuwa imepatikana kwa udanganyifu kuanzia katika fursa za kujiunga na shule, vyuo, kughushi vyeti, kuiba mitihani na rushwa za ngono au pesa katika kupata ajira kama sio kujuana kwamba unamfahamu nani na sio unafahamu nini, wanaotumia lugha ya Kiingereza wanasema ‘Technical know who not technical know how’.
Wapo wengi na kama ikifanyika tathmini bila upendeleo Tanzania inaweza kushangaza dunia jinsi inavyoongozwa na baadhi ya watu ambao kwa hakika leo hii wangestahili kuwa gerezani kutokana na uvunjaji wa sheria waliofanya.
Lakini habari za udangayifu, kuiba mitihani, kughushi vyeti, rushwa za ngono na pesa katika ajira sio ngeni barani Afrika na anayetaka kuwa bingwa wa uhalifu wa aina hiyo basi anaweza kujifunza maarifa hayo Nigeria.
Kitu kinachosikitisha zaidi hapa Tanzania ni kwamba wakati jamii katika nchi nyingine zenye matatizo hayo zinachukizwa wazi wazi na vitendo hivyo, hapa Tanzania wako wengi wanaoona uhalifu huo kama tatizo dogo sana au ni jambo la kawaida.
Kwamba mwanafunzi asiyeweza kukokotoa hisabati rahisi anaweza kupewa alama za juu kutokana na kuiba mitihani na hatimaye akapata fursa mbalimbali za masomo na ajira hadi akawa kiongozi wa jamii.
Mitizamo ya mambo kwa ukaribu, inatokana na ufinyu wa hekima, inayosababishwa na tamaduni mbaya za makabila yetu na elimu duni inayotolewa katika shule za umma.
Hakuna kubisha katika hilo kwani utafiti uliofanywa na Serikali Kuu kupitia Mpango wa Kuinua Uchumi na Kupunguza Umaskni (MKUKUTA) mwaka 2007 kuhusu mtizamo wa wanafunzi wadogo katika elimu na jukumu lao katika jamii uliweka wazi baadhi ya mambo.
Utafiti huo unaitwa kwa Kiingereza “Tanzania Children’s Perception of Education and Their Role in Society: Views of the Children 2007” na ulifanyika Tanzania Bara kwa kuhoji wanafunzi wadogo 500 (umri miaka 7 mpaka 14) katika mikoa kumi (Arusha, Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Singida, Rukwa, Shinyanga na Mwanza).
Watafiti wa MKUKUTA walikusanya maoni ya wanafunzi wadogo kuhusu masuala ya elimu, huduma katika shule zao kama matibabu, maji safi, chakula, vitabu, walimu, nidhamu, uchangiaji elimu na matarajio yao kuhusu uboreshaji elimu. Matokeo ya utafiti huo yanasikitisha.
Kumbe wanafunzi wadogo wanachukia sana shule na walimu wao kiasi kwamba kama wangekuwa huru na hiari ya kujiamulia mambo basi wengi wangekataa kabisa kufika shule wanazosoma.
Kati ya wanafunzi wadogo 500 waliotoa maoni katika ufatiti huo ni wanafunzi 10 (sawa na asilimia mbili) ndio walioonyesha dhamira ya kutaka kuendelea na masomo zaidi.
Lakini cha ajabu ni kwamba wanafunzi 39 (sawa na asilimia tisa) walisema wanapenda kuwa marais wa nchi (kiongozi mkuu wa dola na serikali).
Wanafunzi 38 (sawa na asilimia nane) walisema wanapenda kuwa madaktari wa tiba. Wanafunzi 143 (sawa na asilimia 32) walisema wanapenda kuwa walimu, wakati wanafunzi 15 (sawa na asilimia tatu) walisema wanapenda kuwa marubani.
Hii maana yake ni kwamba katika shule za Tanzania kuna wanafunzi wadogo (miaka saba mpaka 14) wanaotamani kuwa marais, walimu, madaktari wa tiba na marubani lakini hawapendi kuendelea kusoma zaidi. Hayo kama sio maajabu ya kusikitisha ni nini?
Kwa mtu mwenye busara atasema, “Ahh, hayo si maoni ya watoto wa miaka saba hadi 14 tu… bado ni wadogo, hawajui wasemalo…!”
Lakini umri huo ndio unaopendekezwa na serikali kwa watoto wote kuanza masomo ya shule za msingi.
Jawabu linalopatikana hapa ni kwamba idadi kubwa ya watoto wanaokosa fursa ya kuingia shule za sekondari (takribani asilimia 80) hawajutii kukosa elimu hiyo kwani tayari wanachukia shule na walimu.
Watafiti wa MKUKUTA walithibitisha hilo kwa kukusanya maoni yenye sababu tisa za watoto kuchukia shule na walimu wao. Watoto walibainisha kuwa walimu wao ni wakali sana na hufundisha kwa hasira.
Aidha walisema kuwa walimu wao hawasahihishi madaftari yao au wanatumia muda mrefu sana kufanya hivyo na jibu jingine lilikuwa walimu wao wananyanyasa watoto.
Jibu jingine lilikuwa walimu wao wanatuma wanafunzi wenzao kuwaandika “notes” kwenye ubao darasani na walimu wao wakiingia darasani wanaanza kuuliza wanafunzi maswahi hata kabla ya kufundisha lolote, na wanafunzi wanaoshindwa kujibu wanaadhibiwa kwa kipigo.
Majibu hayakuishia hapo walisema walimu wao wanaagiza wanafunzi wadogo waende kujifunza kwa wanafunzi waliowatangulia madarasa na aidha walimu wao wanatoa vichekesho tu darasani na kuondoka bila kufundisha chochote cha maana.
Hali kadhalika walisema walimu wao wanaongea kwa haraka hususan kwa Kiingereza ambacho hawakielewi vizuri na pia jibu jingine likawa kwamba walimu wao wanatuhumiwa kwa tabia mbaya na jamii mitaani.
Hoja inayoibuka hapa ni kwamba je, nini kibaya na hatari zaidi: watoto kuchukia shule na walimu wao au wizi wa mitihani?
Jibu ni kwamba hakuna shaka kuwa yote ni mabaya lakini kipaumbele kiwe wapi ili kuimarisha mapambano dhidi ya adui ujinga.
Kwa kuzingatia maelezo ya watoto hao wapo ambao watakuwa wanajituma na wapo ambao watabakia kuwa wasindikizaji na siku ya mtihani inapofikia ndipo inafikia hatua za kutafuta mbinu za kufaulu.
Walimu kwa upande wao watakuwa wanashiriki udanganyifu huo ili kuondokana na kile ambacho kinaweza kuelezwa kuwa ni aibu ya shule kutofaulisha lakini pia wanaweza kuwepo ambao watafanya udanganyifu huo kutokana na kupokea rushwa kutoka kwa ama wazazi au walezi wa watoto.
Historia inajirudia?
Kabla ya yale yaliyotokea kwenye mitihani ya darasa la saba haijakaa sawa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa watahiniwa wa mwaka jana 2011 nayo yakatolewa ambapo Dk. Ndalichako anasema watahiniwa 3,301 walibainika kufanya udanganyifu na hivyo kufutiwa matokeo na kwamba hawataruhusiwa kufanya mitihani ya baraza hilo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba yaliyojiri kwenye karatasi za majibu ya watahiniwa hao kwa mujibu wa Dk. Ndalichako ni pamoja na kuwepo kwa miandiko zaidi ya 10 kwenye karatasi moja, kukamatwa kwa karatasi za majibu zaidi ya moja.
Mbaya zaidi ni kuwepo kwa utovu wa nidhamu wa kuandika matusi ya nguoni kwenye makaratasi ya majibu pamoja na tenzi za nyimbo za kizazi kipya na michoro isiyoeleweka ya wachezji wa mpira.
Katika mazingira hayo ni kwamba wanaofanya au kufanyiwa udanganyifu huo watamudu kuacha? Haiyumkini jibu linaweza kuwa hapana kwani tabia hiyo inaweza kuwa endelevu na ikaendelea hadi kutinga kwenye sehemu za kazi watakazokuwa au kwenye nyadhifa mbali mbali watakazokuwa nazo.
Hivyo jamii inakuwa tayari inaongozwa na viongozi wadanganyifu, wasio waadilifu, wala rushwa na mafisadi.
Na Tanzania Daima

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII