HABARI MPYA LEO  

Mafisango kuagwa leo

By Maganga Media - May 18, 2012

Hili ndio gari alilokuwa akiendesha Mafisango.Alikua na wenzake wanne kwenye gari ambapo wengine wanne wamepona japo walipata majeraha madogo madogo akiwemo mdogo wake ambae amesajiliwa na club ya Simba.

Aliyekuwa kiungo maili wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi),  Patrick Mutesa Mafisango (pichani) aliyefariki kwa ajali ya gari alfajili ya jana katika eneo la Veta Keko jijini Dar es Salaam, anatarajiwa kuagwa leo asubuhi kuanzia saa 4:00.

Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba Godfrey Nyange Kabulu amesema kuwa mwili wa marehemu Mafisango utaagwa katika viwanja vya Sigara (TCC CLUB), Chang'ombe jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi na kusafilishwa Mei 19 kwenda kwao Congo DRC kwa mazishi.Wazazi wake wanaishi Congo DRC

Mafisango alipata mauti hayo eneo la Veta Chang'ombe usiku wa kumkia jana saa 8.45 alipokuwa akiendesha gari akitokea Maisha Club akiwa na wenzake wanne na alipofika maeneo ya Veta wakati akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli ya miguu mitatu 'Guta' gari lilimshinda na kugonga mti uliosababisha gari yake kuingia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo mtoto wa dada yake Orly Ilemba (24) aliyekuwamo katika gari hilo alisema jana wakati wanavuka mataa ya Veta, marehemu alikuwa katika mwendo kasi mara mbele akakutana na Guta na katika jitihada za kulikwepa akagonga mti na gari kupinduka na kutumbukia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.

"Tulitoka salama Maisha Club tunarudi nyumbani marehemu alikuwa akiendesha gari katika mwendo wa kasi, tulipovuka mataa ya Veta wakati akiwa 'spidi' tuliona guta kwa mbele yetu pamoja na pikipiki sasa wakati marehemu anakwepa kwa bahati mbaya aligonga mti na gari ikadumbukia ndani ya mtaro huku nikishuhudia kichwa cha ndugu yangu kikigeukia chini kwenye sehemu ya breki na miguu kuja juu kumbe tayari alishafariki......ndipo tukaanza taratibu za kumkimbiza hospitali," alisema Ilemba.

Aliongeza kuwa,"ndani ya gari hiyo aina ya Gx100 tulikuwa watu jumla ya watano mimi, Gaspar Karemera, Bozy na mwanamke mmoja ambaye yeye hatukumfahamu jina lake mara moja akiwa amekaa mbele na marehemu ambaye mpaka sasa bado yupo hospitali akiendelea na matibabu baada ya kuumia sana maeneo ya kichwani,"alisema Ilemba.

Akithibitisha kifo cha mchezaji huyo, Mkuu wa Trafiki katika mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Prackson Lugazia alisema  ajali hiyo ilitokea wakati Mafisango aliyekuwa akiendesha gari aina ya GX 100 akitoka Maisha Club akiwa na familia yake akijaribu kumkwepa mwendesha Guta. Hali hiyo ilisababisha gari hilo kuacha njia na kuingia mtaroni na kugonga miti mitatu kisha kugeuka na kuangalia lilikokuwa likitoka na baadaye kupinduka.

Mafisango alijiunga na Simba akitokea Azam Fc, mwaka jana alizaliwa Machi 7, mwaka 1987, nchini Rwanda na alikuwa akiichezea timu ya Taifa ya nchi hiyo kabla ya kusimamishwa kwa muda mrefu kutokana na utovu wa nidhamu na amerudishwa kundini na kocha Micho, lakini hata hivyo hajaweza kuitumikia timu hiyo ya Taifa lake.

Mchezaji huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika timu ya Simba msimu huu uliomalizika hivi juzi na kung'aa zaidi katika Ligi hiyo kwa kupachika mabao na kutoa pasi za mwisho, ambapo Mechi ya mwisho ya Mafisango ilikuwa ni kati ya Simba dhidi ya Al Ahly Shandy Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penati 9-8, kufuatia sare ya jumla ya mabao 3-3.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII