HABARI MPYA LEO  

Dawa mpya ya VVU yaidhinishwa!

By Maganga Media - May 19, 2012


MAMLAKA ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), imeidhinisha dawa ya Truvada kuwa tiba ya kuzuia kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).Dawa hiyo ambayo awali ilikuwa katika kundi la zile zinazotumiwa kwa ajili ya Kupunguza Makali ya VVU (ARV), imepandishwa chati wakati ambapo tayari ipo sokoni ikiuzwa kama moja ya ARV za kawaida.

Kwa mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu na hatomuambikiza.

Matokeo ya utafiti huo yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti la Mwananchi  toleo la Februari 12, mwaka huu na sasa kilichofanyika ni FDA kuidhinisha Truvada ambayo ilionyesha kufanya kazi vizuri ikilinganishwa na ARV nyingine.

Lakini, dawa hiyo masharti yake hayatofautiani na yale ya ARV kwani mtumiaji atapaswa kuitumia maisha yake yote ili kumwekea kinga asiwaambukize wengine na yeye aishi muda mrefu.

Kulingana na ripoti ya utafiti uliofanyika Marekani, dawa hiyo ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU hadi asilimia 90.Hata hivyo, kwa watu ambao wamekuwa wakitumia dawa holela hasa za ARV, hali imekuwa tofauti kwani Truvada imeonekana ikifanya kazi kwa kiwango cha asilimia 44 tu.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII