HABARI MPYA LEO  

Waziri Nohodha kuchunguzwa

By Maganga Media - Apr 16, 2012



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, inayoongozwa na Edward Lowassa imependekeza kuundwa kwa kamati teule ya watu wanne kumchunguza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha kwa madai ya kukataa kutekeleza agizo lake lililotaka nusu ya matrekta ya Kilimo Kwanza yaliyopelekwa Shirika la Uzalishaji Mali la Suma JKT, yapelekwe Magereza.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lowassa alithibitisha kuundwa kwa kamati hiyo ndogo lakini akasema haina madaraka mpaka Spika, Anne Makinda, atakaporidhia.

Chanzo cha habari kutoka bungeni kimeitaja kamati iliyopendekezwa kumchunguza Waziri Nahodha kuwa itawajumuisha Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi, Masoud Salim Abdallah, Hilda Ngoye na Muhammed Seif Khatib.

Msingi wa pendekezo la kamati hiyo unatokana na Jeshi la Magereza kuwa na nguvu kazi ya kuzalisha tofauti na Suma JKT, hali ambayo ingesaidia kuondoa utegemezi wa chakula kwa wafungwa. Inadaiwa kwamba Waziri Nahodha alikataa kutekeleza agizo hilo na alipoitwa tena kwenye kamati ili kueleza sababu zake, anadaiwa kujibu kuwa Magereza hawahitaji matrekta hayo kwa sababu hayana ubora.  “Majibu yake yalionekana kuwa kuna kitu kimejificha nyuma kwa sababu yeye alishiriki kupitisha mpango wa kuagizwa matrekta hayo na alikuwa na fursa ya kulishauri Baraza la Mawaziri lisiendelee na mradi huo kama ni mbovu kama anavyoeleza,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Chini ya mpango huo wa Serikali wenye lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, matrekta 1,860 ya Farm Track kutoka India yameingizwa nchini ikiwa ni mkopo wa Dola 40 milioni za Marekani.Kutokana na Kamati ya Lowassa kutilia shaka majibu ya Waziri Nahodha, kamati hiyo iliwaita makamishna wa Jeshi la Magereza ambao wanadaiwa kutamka kuwa wanayahitaji, lakini kikwazo ni waziri wao.
Msimamo wa Nahodha
Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana, Waziri Nahodha alikiri kushauriwa na Kamati ya Bunge kuhusu suala la kupeleka matrekta Magereza lakini akasema: "Sasa haiwezekani kwa kuwa matrekta yenyewe hayapo."  "Kilichotokea ni kwamba kamati imeishauri wizara yangu inunue matrekta hayo 72 na mimi nimewashauri wao waende wakayaangalie kwanza halafu watushauri ili tukifanya uamuzi uwe wa busara."

Waziri Nahodha alisema kimsingi wizara yake iko mstari wa mbele kutekeleza Kilimo Kwanza na inajipanga kwa hali na mali kuliwezesha Jeshi la Magereza lijitegemee kwa chakula na hata ikiwezekana lianze kuuza chakula hicho.

Hivi karibuni, Serikali ya India ilisema inajipanga ili kuwekeza zaidi Tanzania, kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo ukiwamo huo wa matrekta.

Ahadi hiyo ilitolewa na Kaimu Balozi wa India nchini, Hemalata Bhagirath alipotembelea mradi wa matrekta hayo eneo la Mwenge, Dar es Salaam na kuridhishwa na mafanikio yake.

Alisema lengo la kuletwa nchini matrekta hayo ni kukopeshwa wakulima wa Tanzania ili kufanya mapinduzi ya kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza.

Balozi Bagirathi alisema kutokana na mwitikio mzuri kwa Watanzania kwa matrekta hayo, nchi yake inaweza kuangalia uwezekano wa kufungua kiwanda cha matrekta hayo ili kutosheleza mahitaji ya Kilimo Kwanza.


Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII