HABARI MPYA LEO  

WAKUU WA SHULE WAVULIWA MADARAKA - KIGOMA

By Maganga Media - Apr 23, 2012

 SERIKALI imewavua madaraka wakuu wa shule za sekondari 10 zilizopo Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kuthibitika kuhusika na mpango wa kuwaingiza bila kuwa na sifa kuendelea na masomo ya sekondari kwenye shule za serikali, wanafunzi zaidi ya 350 ambao walifeli mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.

Habari za uhakika kutoka kwa maofisa waandamizi wa Idara ya Elimu Mkoa wa Kigoma ambao   hawakutaka kutajwa majina kwa kuwa si wasemaji rasmi, walisema wakuu hao wa shule za sekondari walivuliwa madaraka yao kuanzia mwanzoni mwa wiki hii na kutakiwa kukabidhi kwa wakuu wa shule wasaidizi.

Shule hizo za sekondari zilizokumbwa na kadhia hiyo ni Mwananchi, Kasingirima, Rusimbi, Kitongoni, Katubuka, Buteko, Wakulima, Mlole na Masanga.

Machi 5, mwaka huu, Mkaguzi wa Shule za Sekondari Kanda ya Ziwa Magharibi, Charles Kawasange aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kuwa zaidi ya wanafunzi 487 ambao hawakufaulu mitihani yao ya darasa la saba, wamekutwa wakiendelea na masomo katika shule 15 za sekondari za Kigoma Ujiji isivyo halali.

Alizitaja shule za sekondari zilizobainika kuwa na wanafunzi hao kuwa ni Buronge, Buteko, Kasingirima, Katubuka, Gungu, Kasimbu, Kichangachui, Wakulima, Mwananchi, Kitwe, Kirugu, Kitongoni, Masanga, Mlole, Rubuga na Rusimbi.

Mkaguzi huyo alisema katika ukaguzi wao waliwahoji wanafunzi wote wa shule hizo kwa mdomo na kutoa madodoso ambapo wanafunzi wengi walikiri kutofaulu mitihani ya darasa la saba na kwamba waliingia katika shule hizo kinyemela katika mpango uliofanywa na wakuu wa shule hizo za sekondari na wazazi wao.

Alisema sababu kubwa ya kufanyika kwa ukaguzi huo katika shule hizo kulitokana na baadhi ya wanafunzi kushindwa kuingia katika vyumba vya mitihani kufanya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana na walipoulizwa, iligunduliwa kwamba hawana taarifa za mwanafunzi za maendeleo ya shule (TSM 9) ambazo hupewa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakuu wa shule za sekondari waliovuliwa madaraka wamekuwa wakihaha kwa kuwatumia watu mbalimbali ili kujinusuru na jambo hilo.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII