HABARI MPYA LEO  

Rais Barack Obama akiwa ziarani Korea Kusini

By Maganga Media - Mar 25, 2012

Obama akiwa 'mpaka wa uhuru'


Rais Barack Obama akiwa ziarani Korea Kusini, amezuru eneo la mvutano la mpaka na Korea Kaskazini.Amewasili Korea Kusini kwa mkutano wa kilele kuhusu usalama wa silaha za nuklia, ikiwa sehemu ya mpango wake wa miaka minne kuzuia zana za nyuklia kufika katika mikono ya wahalifu. Akiwa nchini humo Rais Obama alizuru kituo cha ulinzi karibu na eneo linalotambuliwa na jeshi kuwa linatenga Korea Kaskazini na Kusini. Alitumia darubini kuangalia vijiji ndani ya taifa la kikoministi la Korea Kaskazini.

Hapo awali, alisimama mbele ya wanajeshi wa Marekani, na kuwaambia kuwa wako zamu kwenye "mpaka wa uhuru". Shughuli hizo alizofanya leo asubuhi, baada ya kuwasili tu Korea Kusini, zimekusudiwa kuwaunga mkono wanajeshi wa Marekani walioko huko na kuonesha ushirikiano wa kijeshi baina ya Marekani na Korea Kusini. Pia zinaonesha mvutano ulioko hivi sasa na Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.

Korea Kaskazini haitahudhuria mkutano huo wa kilele mjini Seoul. Mazungumzo nje ya mkutano yanaelekea kuhusika hasa na hitilafu mpya kati ya Marekani na Korea Kaskazini, kuhusu mpango wa Korea Kaskazini kurusha satalaiti angani mwezi ujao. Wakuu wa Marekani wamesema wazi kuwa Rais Obama atalipeleka swala hilo kwenye mazungumzo yake na marais wa Uchina na Urusi.

Maganga Media

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII