HABARI MPYA LEO  

Wafanyakazi kuandamana

By Unknown - Aug 1, 2012

 SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limetangaza maandamano ya amani yatakayofanyika Dar es Salaam wiki hii ili kupeleka malalamiko yake kwa Serikali ya kutokubaliana na sheria mpya ya mafao ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA).
Sheria inayolalamikiwa na wafanyakazi inazuia wanachama wa mifuko hiyo kujitoa uanachama na kuchukua mafao yao mpaka wafikishe umri wa kustaafu kwa hiari wa kati ya miaka 55 na 59 na kwa lazima miaka 60 au wanapopata ulemavu wa kudumu.
Mratibu wa Kamati ya Tucta ya Mkoa wa Dar es Salaam, Musa Mwakalinga jana alisema maandamano hayo yatafanyika Agosti 4 na yataanza saa 1.30 asubuhi katika ofisi za Tucta makao makuu Mnazi Mmoja hadi ofisi za SSRA eneo la Makochi, Kinondoni barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Mwakalinga alisema maandamano hayo yatashirikisha wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima na kueleza kuwa wameshatoa taarifa Polisi kupata ulinzi ili kufikisha kilio chao, kwa kuwa mabadiliko hayo yataongeza umasikini kwa wafanyakazi pindi watakapoachishwa au kuacha kazi.

“Sisi tunachofanya ni maandamano ya amani, hivyo hatuna haja ya kuomba kibali, ila tulichofanya ni kuwapa taarifa tu ili watupe ulinzi,” alisema Mwakalinga.

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema wanabariki maandamano hayo na wanataka mabadiliko ya haraka yafanyike kwenye sheria hiyo ya hifadhi ya jamii, ili fao la kujitoa lirejeshwe.

Alisema wadau na Tucta hawakuona kifungu hicho cha sheria kwa kuwa hakikujitokeza kwa uwazi kwenye muswada au kama ilivyoelezwa na SSRA, baada ya sheria kupita na kifungu pekee cha muswada kilichotaja suala la mafao ya kujitoa ni cha 107 kilichotoa mapendekezo ya kufuta fao la kujitoa kwa mfuko wa PPF.

Hivyo alisema wadau na vyama vya wafanyakazi walielewa kuwa kifungu hicho kinalenga kufuta fao la kujitoa kwa mfuko wa PPF tu, ambao ndio pekee uliokuwa na fao hilo na kwamba malipo ya kujitoa yangeendelea kutolewa kama ilivyokuwa ikifanyika kwa mifuko mingine.

Kutokana na hilo, alisema Tucta inataka uandaliwe utaratibu mwafaka utakaohakikisha mwanachama anayeshindwa kuendelea na uanachama wa Mfuko anarejeshewa michango yake na ya mwajiri pamoja na riba mara tu anapokoma uanachama wa mifuko hiyo.

Alisema Tucta haitasita kuchukua hatua za kisheria, endapo mamlaka itaendelea kushikilia msimamo wake wa kubakiza kifungu hicho kinachomtaka mwanachama wa mfuko afikishe miaka 55 ndipo alipwe mafao.

Aidha, alisikitishwa na kushangazwa kuwahishwa kutangazwa kwa mabadiliko ya sheria ya hifadhi ya jamii, huku mchakato wake ukiwa haujakamilika baada ya kuridhiwa na Rais, kama vile kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali, akisema huo ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu.

“Hali hii inatupa shaka kuwa huenda sheria hiyo ikawa na mabadiliko ambayo wadau hatukuyaridhia, jambo ambalo Tucta kamwe hatutalikubali,” alisema. Alisema Tucta inataka SSRA kuchukua jukumu la kutoa elimu kwa wanachama kuhusu sheria hiyo mpya ili kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII