HABARI MPYA LEO  

Tamko la Serikali kwa tukio la kuzama kwa Meli Ya MV Skagit

By Unknown - Jul 26, 2012




KAULI YA SERIKALI KUHUSU TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA BAHARI YA CHUMBE

Mheshimiwa Spika;

Kwa heshima naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo tukiwa wazima na wenye afya njema. Pili, naomba nichukue nafasi hii adhimu kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kutupatia fursa hii adhimu ili kuwasilisha mbele ya Baraza lako Tukufu taarifa ya maafa ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea katika bahari ya Chumbe tarehe 18.07.2012.

1.0 Utangulizi

Mheshimiwa Spika, Meli ya MV. Skagit ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na imesajiliwa Zanzibar tarehe 25/10/2011, na kupewa nambari ya usajili 100144. Meli hiyo ina uzito wa GRT96 ambayo inamilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Limited ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 18.07.2012 majira ya saa saba na nusu za mchana ilipatikana taarifa ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit katika bahari ya chumbe nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Meli hiyo ilikuwa katika safari zake za kawaida ya kutoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar.

Kwa mujibu wa manifest ya abiria iliyowasilishwa na wamiliki wa meli kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority-TPA) na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu Tanzania (Surface and Marine Transport Authority-SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua jumla ya watu 290 wakiwemo abiria watu wazima 250, watoto 31 na mabaharia 9.

Mheshimiwa Spika, Taarifa hii inaelezea kwa kina juu ya hali halisi ya tukio pamoja na hatua zote zilizochukuliwa kuanzia tarehe 18/07/2012 hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Spika, Mara baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Aidha, Baraza la Mapinduzi lilikaa usiku wa tarehe 18.07.2012, na kutoa maagizo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo kuwepo kwa matayarisho katika hospitali ya mnazi Mmoja ya kupokea majeruhi, kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya mapokezi na utambuzi wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa kwa taarifa rasmi ya hali ya uokozi iliyokuwa inaendelea.

2.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Mheshimiwa Spika Kufuatia maagizo hayo ya Serikali, hatua zifuatazo zilichukuliwa: -

• Vituo cha mapokezi ya wahanga wa ajali hiyo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Malindi, Hospitali ya Mnazi Mmoja na uwanja wa Maisara.

• Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha huduma za ulinzi na uokozi wa haraka.

• Kazi ya uchimbaji wa makaburi katika eneo la Kama ilifanyika kwa mashirikiano makubwa ya viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi. Jumla ya makaburi 80 yalichimbwa.

• Sala na dua maalum ya kuwaombea marehemu wote ilifanyika baada ya sala ya Adhuhuri jana tarehe 22.07.2012 katika misikiti yote ya Unguja na Pemba na Kitaifa ilifanyika katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Zanzibar.

• Kuorodhesha majina ya wale wote ambao wanasadikiwa walikuwemo ndani ya chombo kilichopata ajali na hadi sasa hawajulikani walipo.

Taarifa hizi zinakusanywa kupitia ngazi ya Shehia na Wilaya kwa Unguja na Pemba na kwa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa Tanzania Bara.

• Kutoa huduma ya kuwasafirisha majeruhi baada ya kupata matibabu kurudi makwao. • Kutoa huduma za usafiri kwa walioshiriki katika shughuli zote za operesheni.

3.0 MATOKEO YA OPERESHENI

3.1 Shughuli za uokozi

Mheshimiwa Spika; Kutokana na operesheni iliyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa mashirikiano makubwa ya wananchi yamepelekea hadi kufika tarehe 22.07.2012 kuwa na idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kufikia 146 na miili ya waliofariki dunia iliyopatikana kufikia 73.

Kati ya maiti hizo 68 zilipokelewa kituo cha Maisara na 5 zilipelekwa moja kwa katika eneo la makaburi la Kama kwa vile maiti hizo zilikuwa zimeshaharibika. Kwa waliookolewa wakiwa hai waliweza kufikishwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi na matibabu. Hadi hii leo, majeruhi wote walishatibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.

Mheshimiwa Spika; Katika kituo cha Maisara maiti zilipangwa ili kuwawezesha ndugu na jamaa kutambua maiti zao na kwa kurahisisha kazi hiyo, Shirika la Utangazaji kupitia kituo chake cha Televisheni kilichukua picha za sura za marehemu na kuzionyesha zikiwa tayari zimewekewa namba ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji wa maiti hizo.

Kupitia utaratibu huu, jumla ya maiti 50 zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Idadi ya maiti ambao hawakutambuliwa ni 23 na mazishi yao yalisimamiwa na Serikali katika eneo la Kama.

Aidha, maiti mmoja aliyetambuliwa alilazimika kuzikwa Kama kwa vile mwili wake ulikuwa umeharibika sana sambamba na ndugu wa marehemu huyo kutochukuliwa na jamaa na ndugu zake. Kila maiti alizikwa katika kaburi lake chini ya usimamizi wa mashekhe kutoka Ofisi ya Mufti na Wakfu na Mali ya Amana.

Aidha, katika kituo cha Maisara huduma za uoshaji na sala ya maiti zilitolewa na pia wale wote waliochukua maiti wao walipatiwa usafiri, sanda na ubao kwa ajili ya kuzikia.

3.2 Juhudi za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana

Mheshimiwa Spika,
 Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha miili zaidi ya marehemu iliyotokana na ajali ya meli inapatikana, Serikali ilivitaka vikosi vyake ulinzi na usalama vikiongozwa na KMKM kuendesha zoezi la kuitafuta meli na miili iliyosalia.

Kazi ya kuendesha operesheni ya kuitafuta meli pamoja na abiria ilianza mara tu baada ya kusikia kutokea kwa ajali hiyo. Jumla ya watu waliohai 146 waliokolewa siku hiyo na maiti 31 zilipatikana. Asubuhi ya tarehe 19.07.2012, wazamiaji kutoka KMKM, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na makampuni binafsi walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Wazamiaji hao walifanikiwa kupata maiti 37 na hawakupata abiria aliye hai. Hata hivyo, wazamiaji hao hawakuweza kuiona meli.

Mheshimiwa Spika,
Vikosi hivyo viliendelea na jitihada za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana kwa kujigawa katika makundi matatu. Makundi mawili yalihusika na kazi ya utafutaji wa watu katika maeneo ya ukanda wa eneo la tukio. Kundi jengine lilijihusisha na kazi ya uzamiaji (diving) kwa ajili ya kuitafuta meli chini ya bahari.

3.3 Kukusanya taarifa za watu waliokuwa hawajaonekana kupitia Ofisi za Masheha na Wilaya:

Mheshimiwa Spika, 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliziagiza ofisi zote za Wilaya na Shehia kuorodhesha majina ya watu waliokuwa hawajaoneka na waliofariki na kuziwasilisha orodha hizo kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kufanyiwa uhakiki na kupata orodha sahihi kwa ajili ya matumizi na kumbukumbu za baadae.

Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 zaidi ya watu 100 wameripotiwa hawakuonekana ama wakiwa hai au maiti. Hata hivyo, kwa uhakiki wa awali imebainika kwamba baadhi ya watu wameorodheshwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti.

3.4 Viongozi Wakuu wa Kitaifa kutoa mkono wa pole

Mheshimiwa Spika,
 Viongozi Wakuu wa Kitaifa pamoja na viongozi wengine wanatarajiwa kufanya ziara za kutoa pole na kuzifariji familia zilizofiliwa na zilizopotelewa na ndugu zao kwa maeneo yote yalizoathirika Unguja na Pemba. Kazi hiyo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

3.5 Kuratibu upokeaji wa misaada

Mheshimiwa Spika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa iliendelea kupokea misaada ya kifedha na vifaa kutoka kwa watu binafsi, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 jumla ya Shilingi 320,000,000/-zimepokelewa na kuingizwa katika akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar (Zanzibar Disaster Funds) ilioko Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo imefunguliwa maalum kwa ajili ya michango ya aina hiyo. Aidha, vifaa na bidhaa mbalimbali zimepokelewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za operesheni ya uokozi.

4.0 GHARAMA ZA OPERESHENI Mheshimiwa Spika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipatia Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa jumla ya shilingi milioni ishirini (20,000,000/-) kwa ajili ya kugharamia shughuli za operesheni ambapo hadi kufikia tarehe 22.07.2012 fedha zote zilikwisha tumika.

5.0 TULICHOJIFUNZA KUTOKANA NA TUKIO HILI (LESSONS LEARNED)

Mheshimiwa Spika Kutokana na tukio hili la kuzama kwa meli ya MV. Skagit tumeweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwetu katika kuimarisha kazi na huduma za kukabiliana na maafa nchini. Miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo: –

• Umakini na maamuzi sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na viongozi wetu yameweza kuleta ufanisi mkubwa katika operesheni ya uokozi na hivyo kupelekea kuokoa maisha ya wananchi wetu wengi.

• Muitikio wa haraka wa taasisi mbalimbali za kukabiliana na maafa, zikiwemo taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, Sekta Binafsi na Jumuiya za Kiraia umepelekea watu wengi kuweza kuokolewa wakiwa hai pamoja na kupatikana kwa maiti hali ambayo imewezesha maiti wengi kuzikwa na familia zao.

• Kutokana na wananchi wengi kutumia mtandao wa mawasiliano wa Zantel, kulisababisha ugumu wa mawasiliano kutokana na minara ya kampuni hiyo kuzidiwa na matumizi.

• Udogo wa sehemu ya kuhifadhia maiti (motuary) ulipelekea maiti wasiotambuliwa na jamaa zao kuzikwa haraka na Serikali.

• Uhaba wa vifaa vya kisasa vya uokozi pamoja na wataalamu wa uzamiaji (divers) umepelekea zoezi la uokozi kuwa gumu na kuchukua muda.

• Kukosekana kwa taarifa za uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na wataalamu ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi.

6.0 SHUKRANI

Mheshimiwa Spika Kwa mara nyengine tena kwa niaba ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa naomba nimshukuru Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake kubwa alizochukua ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaokolewa.

Tunamshukuru kwa maelekezo yake na miongozo aliyotupatia ambayo kwa kiasi kikubwa ilitusaidia kufanikisha kazi za uokozi.

Pia, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yao na msaada mkubwa walioutoa katika kukabiliana na maafa hayo.

Aidha, tunamshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda kwa msaada mkubwa aliotupatia kupitia Ofisi yake.

Tunawashukuru pia Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kutupatia miongozo ya mara kwa mara katika jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza athari za maafa yaliyotokea.

Vile vile tunatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Usalama la Taifa kwa maelekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa katika kukabiliana na janga hili na majanga yanayoweza kutokea baadae.

Shukrani za dhati pia zinatolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zao za haraka zilizosaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi.

Pia tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa karibu nasi na kwa michango yao ya hali na mali katika kukabiliana na tukio hili la kusikitisha.

Mheshimiwa Spika Shukrani pia zinatolewa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, angani na nchi kavu kwa jinsi walivyoshirikiana na Serikali katika kulikabili tukio hili.

Wananchi wa maeneo ya jirani hasa wavuvi na wamiliki wa hoteli na kampuni za kitalii wanapewa shukrani za pekee kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu tokea hatua za awali baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli ya Skagit.

Tunashukuru washirika wa maendeleo na wawakilishi wa nchi marafiki kwa jinsi walivyolichukulia suala hili na kutuunga mkono katika msiba huu wa kitaifa.

Vilevile tunazishukuru taasisi za kidini hasa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti kwa kusaidia maandalizi ya mazishi ya marehemu waliotokana na ajali hiyo.

Tunawashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa namna walivyoshirikiana na Kamati.

Tunawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa na wafanyakazi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi chote toka kutokea kwa janga hili.

Tunawashukuru wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kupokea tokeo hili kwa masikitiko makubwa katika kukabiliana na janga hili.

Aidha, tunawashukuru wale wote walioweza kuchangia kwa hali na mali katika msiba huu.

7.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo nawaomba wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee taarifa hii na kutupatia ushauri ili uweze kutusaidia katika harakati za kukabiliana na maafa hapa nchini. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.

Ahsanteni sana ………………………………

MOHAMED ABOUD MOHAMED [MBM]
WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII