HABARI MPYA LEO  

Madaktari waandaa Maandamano

By Unknown - Jul 13, 2012

KITENDO cha Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), kusitisha usajili kwa baadhi ya madaktari waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo (Interns), kimekoleza moto wa mgomo wa madaktari baada ya wanataaluma hao kutangaza maandamano yatakayofanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Kwa muda wa wiki tatu sasa, madaktari wamekuwa katika mgomo wakitaka kuboreshewa masilahi yao na huduma za afya hospitalini, lakini wanataaluma hao walionekana kuchukizwa zaidi baada ya tukio la kutekwa, kupigwa na kutelekezwa porini kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka huku rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi akifunguliwa mashtaka ya kukiuka amri ya mahakama.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila alitaja lengo la maandamano hayo kuwa ni kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe.

Dk Kabangila alitaja sababu ya pili kwamba, ni kulaani kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka cha kutekwa, kupigwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na sababu ya tatu ni kushinikiza Serikali kuunda Tume Huru ya kuchunguza suala hilo, ili wahusika wajulikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema pia kwamba hatua hiyo imekuja kutokana na kitendo cha Serikali kuendelea kuchukua hatua ya kuwafukuza madaktari na kusitishiwa leseni wale waliokuwa chini ya mafunzo, badala ya kusikiliza na kutatua madai yao yaliyolenga kuboresha huduma hiyo nchini.

“Kama mnavyofahamu, mpaka sasa takriban madaktari 400 walio chini ya usimamizi na wale walio kazini wamesitishiwa usajili na wengine kusimamishwa kazi, na haya yanaendelea wakati suala la msingi likiwa mahakamani na pia Tanzania ikiwa na upungufu mkubwa wa madaktari kwa daktari mmoja kuwa na uwiano wa kuhudumia wagonjwa 30,000,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:

“MAT inasikitishwa na dhuluma hii inayoendelea dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe na hivyo inapanga kuitisha mkutano mkubwa kesho (leo) na inatangaza maandamano ya amani ya madaktari na wale wote wenye mapenzi mema na taaluma hii na sekta ya afya kwa ujumla.”

Dk Kabangila aliongeza kuwa, maandamano hayo yatafuata taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi saa 48 kabla ya kuandamana na madaktari wote watavaa makoti meupe na wasio madaktari watatakiwa kuwa na vitambaa vyeupe.

Alisema maandamano hayo ya amani yataanzia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hadi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambako watakabidhi madai yao serikalini.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII