HABARI MPYA LEO  

Kopa Cocacola hiyoooo!!

By Unknown - Jul 6, 2012

TIMU 14 zitakazocheza hatua ya 16 bora ya mashindano ya Copa Coca Cola Jumamosi tayari zimefahamika jana katika mechi zilizochezwa kwenye viwanja vinne tofauti.

Timu hizo ni Tanga, Mjini Magharibi, Morogoro, Mwanza, Mara, Dodoma, Kinondoni, Temeke, Ruvuma, Kigoma, Rukwa, Arusha, Kagera na Kilimanjaro.

Mechi za kupata timu mbili za mwisho ili kucheza hatua ya 16 bora zinawaniwa na Pwani yenye pointi saba, Singida (7), Tabora (6) na Kusini Unguja yenye pointi nne.

Katika mechi za jana Tanga iliigaragaza Kaskazini Pemba mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam na kupata nafasi moja kutoka kundi B.

Mabao ya Tanga yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 30, 55 (penalti) na 58 wakati lingine lilifungwa dakika ya 53 na Issa Mwanga.

Kwa ushindi huo, Tanga ilifikisha pointi tisa na kuungana na timu za Mjini Magharibi zenye pointi 13, Morogoro pointi 12 na Mwanza pointi 11 kutoka kundi B kucheza hatua ya 16 bora.

Mara yenyewe iliichapa Mtwara mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam na kufikisha pointi tisa hivyo pia kupata tiketi ya 16 bora kutoka kundi C ikiungana na Dodoma yenye pointi 12, Kinondoni pointi 11 na Temeke pointi tisa.

Mabao ya Mara ambayo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa mabao 3-0 yalifungwa na George William dakika ya pili, Edson Mwara dakika ya 17 na 45 na Hassan Ally dakika ya 88.

Mtwara walipangusa machozi dakika ya 36 kwa bao la Ramadhan Njunja.

Ndoto za Ilala kucheza 16 bora ziliyeyuka baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya vinara wa kundi A Ruvuma kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani.

Mbali ya Ruvuma iliyofikisha pointi 16, timu nyingine zilizopata tiketi ya 16 bora kutoka kundi hilo ni mabingwa watetezi Kigoma wenye pointi 12, Rukwa pointi kumi na Arusha pointi nane.

Kagera ambayo jana iliifunga Shinyanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu ni moja kati ya timu mbili ambazo ziliingia 16 bora kutoka kundi hilo.

Nyingine ni Kilimanjaro iliyoongoza kwa kufikisha pointi 18 ikifuatiwa na Kagera yenye pointi tisa.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII