HABARI MPYA LEO  

CHADEMA yafunika Dar!

By Maganga Media - May 27, 2012


Mh.Freeman Mbowe mwenyekiti wa CHADEMA taifa akitoa hotuba yake yenye hamasa kubwa.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kiliteka jiji la Dar es Salaam kilipofanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani kwa lengo la kuzindua mkakati wake mpya unaojulikana kama ‘Movement For Change-M4C’ (Harakati za kuleta mabadiliko) ukiwa na lengo la kukiandaa chama hicho kuongoza dola mwaka 2015.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaonya watu aliowaita wasaliti ndani ya chama hicho, kwa kuwataka wajirudi mara moja, vinginevyo watashughulikiwa  kwa  mujibu wa taratibu.

Hivi karibuni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda amekuwa akizozana na viongozi wa chama hicho tangu pale alipotangaza nia yake ya kuwania urais huku akimtaja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwa atakuwa meneja wake wa kampeni.  Bila kumtaja jina, Mbowe alianza kwa kutoa kauli zilionekana moja kwa moja kumjibu Shibuda, akisema wapo watu wanaodai kuwa Chadema ni chama cha udini na ukabila na kusisitiza kuwa huo ni uzushi. 

Mbowe, Katibu wake Dk Slaa, wabunge na viongozi wengine walifika katika viwanja hivyo saa 9:30 na kufanya umati mkubwa uliokuwepo eneo hilo kulipuka kwa shangwe.  Wabunge waliotia fora katika mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Ubungo John Mnyika tangu alipoingia uwanjani hapo na hata alipopewa nafasi ya kusalimia alishangiliwa kwa nguvu.

Mnyika ambaye hivi karibuni alishinda kesi yake ya ubunge iliyofunguliwa na mpinzani wake kutoka CCM Hawa Ngh’umbi, alisema kesi hiyo imedhihirisha kuwepo kwa mfumo mbovu wa uchaguzi na kwamba madai yake kwamba CCM kimekumbatia mafisadi ni ya kweli.  Aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema naye alishangiliwa kwa nguvu hasa pale aliposema ni heri kuwa na vita vya kudai haki kuliko kuwa na amani inayopumbaza. 

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na vyama marafiki kutoka nchi 16 za Afrika na baadhi ya viongozi kutoka chama tawala cha Ujerumani cha CDU.  Chadema pia kiliendesha kampeni za ‘Vua gamba vaa gwanda’ ambapo kilivuna wanachama wapya 3,120 waliorudisha kadi zao wengi wakitoka CCM.  Awali Chama cha CDU kiliendesha semina kwa viongozi wa Chadema kuhusu matumizi ya vifaa vya elektroniki katika  masuala ya uchaguzi.  

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII