HABARI MPYA LEO  

Kesi ya Lulu yapigwa kalenda

By Unknown - Jul 24, 2012


KESI ya msanii wa fani ya filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, imeahirishwa hadi Agosti 20 mwaka huu, kutokana na Jaji anayeisikiliza, DK Fauz Twaib, kuwa na majukumu mengine.Akiahirisha kesi hiyo jana, Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi, alisema Jaji DkTwaibu, anakabiliwa na majukumu mengine.

“Jaji Twaib ni Mwenyekiti wa Baraza la Kodi na pia ni Mwalimu wa Sheria katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivyo kwa sasa anatekeleza majukumu mengine katika nafasi hizo.Kwa hiyo kesi hiyo inaahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu,” alisema Msumi.

Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, yanayodaiwa kufanyika April 7 mwaka huu nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kesi hiyo ya msingi haijaanza kusikilizwa, tayari imeshafikia ngazi ya Mahakama ya Rufani, baada ya kuibuka kwa utata wa umri wa mshtakiwa huyo.

Utata huo uliiobuka baada ya mawakili wanaomtetea msanii huyo, kuomba kesi isikilizwe katika Mahakama ya Watoto kwa madai kuwa mteja wao bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama, inavyoonyesha katika hati ya mashtaka.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII