Kenya kuomboleza kifo cha Saitoti kwa siku 3
By Maganga Media - Jun 11, 2012
Kenya imetangaza siku tatu za maombolezi baada ya kifo cha Waziri wa Usalama wa Kenya, Profesa George Saitoti, na naibu wake, Orwa Ojode, kwenye ajali ya helikopta ya polisi katika eneo la Ngong, nje ya Nairobi.
Raia wa Kenya walikuwa na masikitiko Jumapili, baada ya taarifa ya ajali hiyo kujulikana, na watu wamekuwa wakizuru nyumba ya kuhifadhi maiti mjini Nairobi kutoa heshima zao. Makamo wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, alipofika kwenye tukio la ajali alitoa rambi-rambi zake na alieleza wale waliokuwamo ndani ya ndege ambao wote wameteketea: "Ndege hiyo ya aina ya Eurocopter ya police airwing, ambayo ilikuwa inaelekea Yugis, ilikuwa imembeba Waziri George Saitoti, naibu waziri Orwa Ojode na maafisa rubani wa ndege, Nancy Gitwanja na Luke Oyugi, na vilevile askari wawili ambao wanakuwa wanaandamana na Waziri Saitoti, Inspector Tonkei na Thomas Murimi"
Rambi-rambi zimekuwa zikimiminika nchini Kenya, pamoja na za Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ambaye alipatanisha baada ya ghasia za uchaguzi uliopita nchini kenya. Profesa Saitoti alikuwa akizungumza kwa ukali dhidi ya al-Shabaab na inaaminiwa alihusika na uamuzi wa jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka jana.
Bwana Saitoti aliwahi kuwa makamo wa rais na waziri wa fedha katika serikali ya Rais Moi, na akitarajiwa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao. Alikuwa na umri wa mika 67.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII