Okwi ruksa kuondoka Simba
By Maganga Media - Jun 7, 2012
KLABU ya Simba imesema iko tayari kumruhusu mshambuliaji wake wa kimataifa toka Uganda, Emmanuel Okwi kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini hilo litawezekana iwapo klabu itakayomuhitaji itakubali kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 500,000 (Sh1.3 Bilioni).
Okwi aliyetoa mchango mkubwa na kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu, amepata ofa ya kwenda kufanya majaribio katika nchi tatu, Uingereza, Serbia na Austria.
Akiongea jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema kimsingi klabu yake imekubali maombi kutoka nchi hizo ili nyota huyo aende kufanya majaribio. "Kwa kuzingatia sera ya klabu, tumekubali maombi hayo na tuko tayari kumruhusu Okwi kwenda kufanya majaribio wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo," alisema Rage.
"Kumekuwa na maneno mengi kuhusu Okwi, hapa napenda kutoa ufafanuzi sahihi kwamba, tumepokea maombi ya mawakala kutoka Uingereza, Serbia na Austria akihitajika kwenda kufanya majaribio," aliongeza.
Wolfgang Strainwender, wakala raia wa Austria ndiye ameonyesha kumuhitaji haraka Okwi baada ya kumwona kwenye mchezo kati ya Uganda na Angola uliokwisha kwa sare ya bao 1-1, huku bao la Uganda likitumbukizwa wavuni na Okwi, alifafanua Rage. "Wakala wa Uingereza na Serbia hawajasema wanamuhitaji haraka kiasi gani. Nadhani kufikia kesho jioni tutakuwa kwenye nafasi ya kufahamu ni lini atakwenda Austria," alisema Rage.
Wakati huohuo, Rage alisema kikosi chake kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam, Juni 15 kikiwa na wachezaji 25 kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kucheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Toto Africans. Baada ya mechi hiyo msafara wa Simba utakwenda Mwanza ambako pia utacheza mechi nyingine ya kujipima nguvu Juni 17.
Wakati huohuo, Rage alisema kikosi chake kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam, Juni 15 kikiwa na wachezaji 25 kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kucheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Toto Africans. Baada ya mechi hiyo msafara wa Simba utakwenda Mwanza ambako pia utacheza mechi nyingine ya kujipima nguvu Juni 17.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII