HABARI MPYA LEO  

Ligi kuu Bara kuanza Septemba mosi

By Unknown - Jun 24, 2012

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba, washindi wa pili na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC 'zitabariki' hekaheka za ufunguzi wa msimu mpya wa ligi kwa kukutaka katika mchezo wa Ngao ya Hisani Agosti 25, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pazia la ligi limepangwa kuanza Septemba Mosi, huku Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikitarajia kuanza Septemba 15 mwaka huu.
Afisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Boniface Wambura, alisema tatiba kamili ya ligi inatarajia kutolewa Julai 23 na kusisitiza nidhamu na heshima wakati wa kipindi cha usajili kwa sababu usajili huo pia utatymika kwenye michuao ya Kombe la FA.

"Hakutakuwa na kipindi kingine cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa dirisha dogo Novemba," alisema Wambura.

Aidha, Wambura alisema kipindi cha kwanza kwa ajili ya usajili wa wachezaji kwa msimu ujao kimeongezwa muda.
Awali, muda uliopangwa ulikuwa ufikie tamati Juni 30, lakini sasa muda huo umesogezwa mbele mpaka Agosti 10, na hiyo ni kwa sababu ya mlinganisho na kalenda ya Matukio ya TFF kwa mwaka 2012/2013.

Wakati huohuo, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18 za sasa.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema lengo la mabadiliko hayo kuchezwa kwa kanda, hivyo msimu huu timu mbili zaidi zitaongezwa ili kufikisha idadi ya timu 20.

"Hii haitahusisha timu tatu zilizokwisha panda daraja ambazo ni Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza Kituo cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na Polisi Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma," alisema Wambura.

Alisema Kamati ya Utendaji pia imepitisha mapendekezo ya kuchezwa mchujo ili kupata timu mbili zitakazoongeza idadi ili kufikia timu 20.

Timu tatu zilizoshuka katika Ligi Daraja la Kwanza ni AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es Salaam, wakati zilizoshika nafasi za pili katika Ligi ya Taifa ni Kurugenzi ya Iringa, Mwadui ya Shinyanga na Tessema ya Dar es Salaam.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII