HABARI MPYA LEO  

NECTA YAPUNGUZA ADHABU

By Maganga Media - May 2, 2012

BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta), limepunguza adhabu ya kufutiwa matokeo watahiniwa 3,303 wa kidato cha nne mwaka 2011, waliobainika kufanya udanganyifu na kufungiwa kufanya mtihani kwa miaka mitatu, sasa watatumikia kifungo hicho kwa mwaka mmoja.

Tamko la Necta limekuja wiki chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwaahidi wabunge kuwa Serikali itawasiliana na baraza hilo na kuangalia uwezekano wa kupunguza adhabu hiyo.

Pinda alisema hayo kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), kuitaka Serikali iwasamehe wanafunzi hao ambao aliwaelezea kuwa kitendo cha kuwafutia matokeo kilitosha kabisa na sasa waruhusiwe kurudia mtihani.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, alisema jana kuwa baraza limechukua hatua hiyo baada ya kutathmini maombi mbalimbali yaliyotolewa na wakuu wa shule, wanafunzi waliofutiwa matokeo, wazazi wao na wadau wengine.

Hata hivyo, Dk Ndalichako hakueleza iwapo hatua hiyo wameichukua baada ya shinikizo la Serikali.
“Wadau wengi walikiri kosa, lakini waliomba kupunguzwa kwa adhabu ya kutofanya mitihani kwa miaka mitatu… Wakuu wa shule na watahiniwa husika wameahidi kuwa iwapo watapewa fursa hiyo watakuwa makini zaidi kuhakikisha wanazingatia taratibu za mitihani,” alisema Dk Ndalichako.

Kwa sababu hiyo, Dk Ndalichako alisema Necta imewaruhusu wafanye mtihani kama watahiniwa wa kujitegemea mwaka 2013, kwa sababu mwaka huu wameshachelewa katika mchakato wa usajili.

“Uamuzi wa Baraza umezingatia kuwa kitendo cha watahiniwa na wadau wengine walioathirika na adhabu hiyo kuomba msamaha kimeonyesha kuwa wametambua athari zinazoweza kutokea kutokana na kufanya udanganyifu,” alisema.

Necta ilitoa adhabu hiyo kwa wanafunzi hao wa kidato cha nne mwaka 2011, baada ya kufanya kikao Februari mwaka huu na kuthibitisha kuwa walifanya udanganyifu kwenye mitihani mbalimbali waliyofanya.
Licha ya kutoa msamaha, Dk Ndalichako alisema Necta itaendelea kutoa adhabu kali kwa wale ambao itabaini wamefanya udanganyifu kwenye mitihani.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII