HABARI MPYA LEO  

Kilichomliza Rage akisoma risala kumuaga Mafisango

By Maganga Media - May 21, 2012



MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameanika kilichomliza wakati wa kusoma risala kwenye zoezi la kuaga mwili wa kiungo wa timu hiyo, Patrick Mafisango kwenye viwanja vya TCC, Chang’ombe juzi, jijini Dar es Salaam. Baada ya kufika katikati, Rage alijikuta akilemewa na simanzi hadi kuangua kilio, hivyo risala hiyo kusomwa na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu,’ hali ambayo ilizidi kuongeza huzuni kwa wengi.

Alisema, Mafisango aliyekuwa akichezea Simba kwa mkopo akitokea Azam, baada ya timu kurejea kutoka Sudan, alimfuata na kumweleza kuwa, kama watamtema, yu tayari kuchezea timu hiyo bila kulipwa. “Ukweli ni kwamba, kilichoniliza hasa ni pale nilipokumbuka kauli yake ya mwisho ya kuniambia maadamu mkataba wake umeisha, ni bora aendelee kuichezea Simba hata bure kutokana na mapenzi yake kwa Simba,” alisema Rage na kuongeza: “Ni vigumu kumsahau mchezaji wa aina hii.

Rage alisema, alipotafakari utayari wa Mafisango kucheza Simba bure, kitendo cha kuomba radhi kwa staili ya kipekee na umati uliokuwa unazidi kufurika kuaga mwili wake, akajikuta ameshindwa kuendelea kusoma risala. Alisema, wakati Simba ikiwa kambini kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya ES Setif ya Algeria katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, Mafisango alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Rage alisema nyota huyo alifanya kitu cha kishujaa ambacho hajapata kukiona, baada ya kwenda kambini Bamba Beach na kuwaomba msamaha wachezaji wanzake na benchi la ufundi chini ya Milovan Cirkovic. Alisema, baada ya kufanya hivyo, Mafisango alifunga safari hadi nyumbani kwake (Rage), na kumwomba msamaha kwa kosa ambalo alilokuwa ametenda, kitu ambacho si cha kawaida kwa wachezaji walio wengi.

Aidha, Rage alisema kuelekea mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Mafisango alimwendea na kumweleza kuwa angemfurahisha kwa kucheza vizuri katika mechi hiyo, ikiwezekana kufunga mabao hadi wamtambue yeye ni nani. “Kabla ya mechi ya Yanga, alinifuata na kunieza: “Mwenyekiti lazima nikupe raha baada ya mechi kwa kuwashindilia Yanga mabao mpaka wakome; wanitambue mimi ni Mafisango,” alisema Rage akimnukuu nyota huyo anayezikwa leo kwao DR Congo.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII