HABARI MPYA LEO  

Jarada la Nassari kwa DPP

By Maganga Media - May 10, 2012

JALADA la uchunguzi dhidi ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wenzake, waliokuwa wakihojiwa na polisi kuhusu kauli walizotoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Arusha Jumamosi iliyopita, limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kwa uamuzi zaidi.

Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Ufuatiliaji n a Tathmini, katika Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issaya Mngulu alisema jana kuwa tayari jeshi limekamilisha uchunguzi na mahojiano na viongozi hao wanaokabiliwa na tuhuma zinazoangukia katika kifungu cha 63 B cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Kwa mujibu wa sheria, kifungu hicho kinahusiana na makosa ya kuhamasisha chuki miongoni mwa jamii kwa kuibua tofauti za matabaka kidini, kikabila, rangi au maeneo na anayekutwa na tuhuma hizo anaweza kushtakiwa kwa makosa ya uchochezi.Mngulu alisema wakati polisi wakisubiri maelekezo kutoka kwa DPP,Nassari na wenzake wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao baada ya kuwekewa dhamana kwa ahadi kuwa wataitwa wakati wowote kama watahitajika.

Pamoja na Nassari, kiongozi mwingine wa Chadema aliyehojiwa kwa zaidi ya saa tisa juu ya
maneno hayo ni, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche na mwanachama Ally Bananga.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII