HABARI MPYA LEO  

TANZANIA yaporomoka FIFA

By Maganga Media - Apr 11, 2012


WAKATI Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) likitarajiwa kutangaza orodha ya viwango vya ubora leo, Tanzania inategemea kuporomoka tena kwa mwezi wa saba mfululizo toka nafasi 141 mwezi uliopita mpaka 145 mwezi huu. 


Kuendelea huko kuporomoka kwa Tanzania, kunaifanya kushika nafasi ya tatu kwa ubora toka mkiani kwa kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Ili timu ijukusanyie pointi inazotakiwa na Fifa, lazima kwanza icheze mechi ya kirafiki ya kimataifa, kucheza mechi za kufuzu na fainali za Kombe la Dunia, pia kushiriki katika mashindano ya kufuzu na fainali za mabara husika.

Kwa mujibu wa viwango vipya vitakavyotolewa kesho na Fifa, Tanzania ipo katika nafasi hiyo baada ya kupata pointi 215, mwezi Machi ilikuwa na pointi 228 katika nafasi ya 141.

Katika orodha hiyo inayopatikana kwenye tovuti ya viwango vya ubora wa soka, inaonyesha kuwa mabingwa wa Cecafa, Uganda wenyewe wapo nafasi ya 92 kwa pointi 362, wakifuatiwa na Rwanda iliyokusanya pointi 327 katika nafasi 105, wakati wapinzani wa Tanzania kwenye harakati za kufuzu kwa fainali ya Mataifa ya Afrika 2013, Msumbiji wenyewe wanashika nafasi 106.

Sudan wapo nafasi 113,  Kenya (117), DR Congo wanakamata nafasi 119, Burundi ipo nafasi ya 127 na Ethiopia (138). Nyingine za Cecafa ni Eritrea (190), Somalia (191) na Djibout inaburuza mkia ikiwa 197.
Mabingwa Afrika 2012, Zambia wenyewe wamepanda kutoka 41 hadi 40 na Mali imesogea hatua moja hadi 41 na kufanikiwa kuingia kwenye tano bora ya bara hili. Libya yenyewe itapanda kutoka nafasi ya 53 hadi 46.

Katika orodha hiyo inaonyesha timu 10 za juu zitabadilika isipokuwa Hispania pekee. Ujerumani itapanda nafasi ya pili, Uruguay itashika  namba tatu na Uholanzi kwa mara ya kwanza tangu 2010 itashuka hadi nafasi ya nne, wakati Italia itaondoka kwenye 10-bora na nafasi yake kuchukuliwa na Denmark.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII