HABARI MPYA LEO  

Kifo cha Kanumba, polisi na waombolezaji!

By Maganga Media - Apr 11, 2012

Na Charles Kayoka

Steven Kanumba


Leo tunamzika shujaa wetu wa maigizo na filamu! Amekufa bado kijana mwenye  nguvu na ndoto nyingi, na jamii ya Watanzania na tasnia ya sanaa ikiwa na matarajio makubwa sana kwake kama ilivyo kwa wasanii wengi waliohai. 
Siwezi kusema ni kazi ya Allah, kwa sababu huwa sipendi kusema hivyo! Ninasema tu kuwa kifo kimetokea na tunapaswa kuwa pamoja katika tukio hilo.

Kwa sisi tulio nje ya nchi taarifa tunazozipata kuhusu mazingira ya kifo chake yanasababisha maswali mengi. Kuna Facebook post iliyosema alikufa Collosseum Gymnasium. Kuna waliomnukuu ndugu aliyesema kuwa alikufa nyumbani baada ya ugomvi na mpenzi wake- Elizabeth Micheal- Lulu. Na haijulikani kama alikufa akiwa nyumbani, au akiwa njiani kuelekea hospitali. Mimi nina maoni haya!
Kwanza nawalaumu Watanzania wenzangu wengi wenye uchungu halali kwa kuamua kumrundikia Elizabeth Micheal makosa na kuweka kwenye FAcebook picha zinazooanisha tukio na uwepo wake, na picha ambazo nyingi ni za nusu utupu, kama vile kusema (ukisoma mengi ya maoni ya awali ya Facebook) huyu ndiye shetani. 
Na kwa kweli, kuna ingizo moja la mtu ninayemheshimu sana lilikaribia  kusema hivyo. Nataka niseme kuwa Lulu ni zao la ujenzi- social construction, ambalo limefanywa na sisi wenyewe, na hasa wanaume. 
Namkumbuka mtoto huyu alivyoanza na baadaye wanaume machangu papa walivyoanza kumnyemelea, kumrubuni na kumjengea sura hii aliyo nayo leo.
Hakuna mwanamke anakuwa “Malaya”- kama kweli neno hilo lina maana, bila kuwepo wanaume. Wanaume ndio wafadhili wa hao wanaokuja kuitwa Malaya baaaye. 
Lakini ikifika wakati mwanamke sasa anasema niko tayari kwa kila mmoja- yaani kwa kila mwanaume, tunajitenga, na kusema fulani ni Malaya- lakini sisi ndio tulioanzisha na kumfanya yeye awe hivyo. 
Siamini kama Elizabeth Micheal alijitengeneza, tulimtengeneza, sisi wanaume na nyie wanawake wenzake. Wanawake wangapi wajitokeze waseme kuwa walikuwa karibu naye tangu wakati manyang’au walipoanza kumnyemelea, wakimshauri awe mwangalifu. Nimeona mara nyingi wanawake husifiana kwa kulipa kwa mwili, sura, maumbile, rangi ya ngozi, na kadhalika. 
Lakini wanapokuja kuharibika au kuharibiwa, lawama zinamwendea anayeonekana kuwa ameharibika.  Hatukuwa na sababu ya kumtundika Lulu kama tulivyofanya, tumetumia fikra mgando kudhani wanawake ndio chanzo cha matatizo. 
Ninawafahamu watu kadhaa, ambao wana heshima zao , waliochangia kumfikisha Lulu hapo alipo, lakini kwa sasa wako kimya. Sisi wengine tumechukulia hili la kuulaumu upande mmoja ni kama unyanyasaji wa kijinsia na mwendelezo wa fikra kuwa mwanamke ndio daima chanzo cha kuanguka kwa mwanaume. dhana ya Femme Fatale- yaanii mwanamke mrembo ni hatari ya kifo- ni kushindwa kuona ukweli kuwa mwanamume ndiye aliyejipeleka kwa mwanamke anayedhaniwa hatari. Kwa hiyo kila mtu anahusika na maamuzi yake.
La pili ni kuhusu polisi wetu. Nilidhani kuna umuhimu wa polisi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na matukio kama haya. 

Kwanza, kama Kanumba alifariki nyumbani kabla ya dokta wake kufika, na walipofika waliamua kupeleka maiti Muhimbili, ilikuwa ni makosa makubwa.
Nini kilichowafanya wawe na haraka hivyo kabla ya kuita polisi. Polisi walitakiwa kuja nyumbani kuchukua ushahidi wa mapigano kama kweli yalikuwapo. Kuchunguza mwili na kuupiga picha pale pale, na kuchunguza mengi ambayo mtu wa kawaida huwezi kuyatilia mashaka. 
Ilinishangaza kuwa polisi hawakumkamata na dokta wake, nasikia ndugu alikamatwa akaachiwa, na kuwa Lulu alikuwa ameitwa kujieleza na amegoma kuzungumza awali akitaka mwanasheria awepo – ilikuwa sahihi kwani sheria inamruhusu. 
Pili, ilinishangaza kuona kuwa polisi hawajafuatilia maoni kwenye Facebook na kutoa rai kwa waomblezaji kuwa isingekuwa vizuri kwa wananchi kuanza kutoa hukumu dhidi ya mtu fulani au kundi fulani, wakati uchunguzi unaendelea. Imetokea mara nyingi kumsingizia mtu ushiriki katika tuhuma , lakini kwa kutumia ushahidi usio na vielelezo. 
Kuua sio kuwepo karibu na marehemu, hatujui nini kilimfanya marehemu aanguke; kama waligombana hatujui kama ni kweli, na kama ni kweli sijui kama kulikuwa na kusukumana au kutupiana vitu;  polisi walitakiwa kuwa na maelezo juu ya hilo, na uchunguzi wa daktari ungefafanua zaidi. 

Ilikuwa ni ghafula tu waombolezaji wakaanza kumuona Lulu kama aliua, na wengine kiasi cha “kumtemea” mate na kusema tulijua angefikia hapo. Polisi walitakiwa kuingilia kati.
Tangazo moja kwenye redio na TV lingezuia mwenendo huu wa maoni na kusubiri mwisho wa uchunguzi. Sijaona maoni kutoka kwenye magazeti pendwa, naomba allah yasichukue mkondo wa kubuni mambo kwa ajili tu ya kutaka kuuza.

mohamedmusta@gmail.com, 0766959349

CHANZO: NIPASHE




MSANII Elizabeth Michael (Lulu)

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII