HABARI MPYA LEO  

ATC haina ndege inayoruka

By Maganga Media - Apr 11, 2012



Sasa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) halina ndege hata moja inayoruka. Hali hiyo inatokana na kuanguka wa ndege yake pekee juzi katika uwanja wa ndege wa Kigoma wakati ikiruka kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kupitia Tabora. Abiria 35 na wafanyakazi wanne wa ndege hiyo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo Ft.119 waliponea chupuchupu kufa katika ajali hiyo.

Hali hiyo imeifanya ATCL kubaki bila ndege kutokana na ndege yake nyingine moja kuwa katika matengenezo kwa muda mrefu sasa. Kutokana na hali hiyo, sasa shirika hilo halitatoa huduma za usafiri hadi hapo litakapopata ndege nyingine.

Juzi baada ya kutokea ajali hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba, alisema wizara yake imewapa mamlaka ATCL ya kwenda katika shirika lolote kukodi ndege ili kuziba upungufu huo.  Mfutakamba alisema ATCL inaweza kutoa mapendekezo kwa wizara kuhusiana na hatua gani zichukuliwe kama ni matengenezo ya ndege ama kutafuta ndege mbadala.

Jana shirika hilo lilisema kuwa limepata hasara kufuatia ndege yake kuanguka mkoani Kigoma juzi na kuharibika. Shirika hilo lilisema kuwa, ndege hiyo haifai tena kwa ajili ya kubeba abiria na kwamba linafanya mpango wa kupata ndege za kukodi ili ziendelee kutoa huduma.

Kadhalika, shirika hilo lilisema kuwa licha ya kupata ndege za kukodi, lakini pia lina mpango wa kufanya biashara kwa ushirika na watu wengine ili kuhakikisha linaendelea kutoa huduma kwa wateja wake.

Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Paul Chizi, alisema ndege hiyo haifai tena hata ikifanyiwa matengenezo. Kuhusu abiria waliokuwa wamekata tiketi kwa ajili ya kusafiri na ATCL, Chizi, alisema watatumia ndege za kukodi za shirika la Precision Air ili kuhakikisha wote wanasafiri kama ilivyokuwa imepangwa.

“Hawa abiria wetu waliokuwa wamekata tiketi za shirika letu watasafirishwa kama ilivyopangwa kwa kuwa hatuwezi kuwaacha na tutawaleta kwa kutumia ndege za shirika la ndege la Precision Air,” alisema Chizi.

Akizungumzia uhai wa shirika hilo, Chizi, alisema haliwezi kufa kwa kuwa wana mipango mingi ya kuhakikisha linafufuka, ikiwemo kumalizia matengenezo ya ndege moja waliyobaki nayo ambayo inatajaria kuanza kutoa huduma zake baada ya wiki tatu zijazo.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII