HABARI MPYA LEO  

KANUMBA AFARIKI DUNIA

By Maganga Media - Apr 7, 2012

 
Taarifa zilizopatikana sasa hivi kutoka kwa mwigizaji Dino, ni kwamba kweli mwigizaji STEVEN KANUMBA amefariki dunia ghafla nyumbani kwake maeneo ya Sinza Vatican, Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo. Inaaminika chanzo cha kifo chake ni baada ya kuanguka na kuanza kutoa mapovu hapohapo nyumbani kwake, alikua akiishi na mdogo wake anaitwa Fetty aliekua chumba kingine ambae amethibitisha kweli kwamba alimkuta kaka yake akiwa ameanguka.
Polisi wameondoka nyumbani kwa Kanumba muda mfupi uliopita baada ya kuwachukua waliokua wanaishi na Kanumba akiwemo mdogo wake Fetty ili kwenda kusaidia maelezo ya kilichotokea.

Bado watu wanazidi kuongezeka nyumbani kwa Kanumba ambapo tayari idadi kubwa ya wasanii wenzake wamefika pamoja na watu mbalimbali, millardayo.com itaendelea kukufahamisha kinachoendelea kadri taarifa zitakavyozidi kupatikana.

Alipelekwa hospitali Muhimbili ambako muda mfupi baadae alifariki dunia, mwili wake bado uko katika chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili hospital. Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ni Gabriel Mtitu na Katibu wa kamati ya mazishi ya muigizaji huyo ni William Mtitu katibu.

Taarifa kamili zitatolewa baada ya uchunguzi wa polisi juu ya kifo chake kukamilika. Chanzo kimesema kuwa Kanumba alifariki wakati akiwa anagombana na mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Lulu. “Alikuwa anagombana na Lulu. Lulu akamsukuma Kanumba, akaangukia kichwa, ndio akafa, ilikuwa saa tisa usiku,”kilisema chanzo.

HISTORIA  YA MAISHA YAKE

Steven Charles Kanumbaa alizaliwa Januari 8, mwaka 1984 mkoani Shinyanga kabla ya umauti kumfiia Aprili 6, mwaka 2012.
 
Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary. Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
 
Ni ni wakati huo akiwa Jitegemee Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam. Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
 
Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.
 
Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.
 
Hivi karibuni, alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015. Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
 
Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
 
Nigeria sasa wanaijua Tanzania katika filamu. Nchi nyingi za Afrika zinaijua sasa na hii ni sehemu ya kazi nzuri ya Kanumba.
 
Mwenyewe aliwahi kukaririwa alifika hadi Hollywood hadi Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa mwili wa marehemu upo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
 
Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin. 


Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII