HABARI MPYA LEO  

EAC wakubaliana juu ya Ulinzi

By Maganga Media - Apr 30, 2012


WAKUU wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameridhia na kusaini itifaki ya ushirikiano katika masuala ya ulinzi na kuelekeza kuanza mara moja kwa majadiliano ya pamoja yatakayopelekea kukamilika kwa mkataba wa pamoja katika masuala ya ulinzi.

Mbali na kutia saini itifaki hiyo, wakuu hao waliipokea ripoti iliyowasilishwa kwao na Baraza la Mawaziri na kuridhia masuala mbalimbali katika ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na kumteua Jesca Eriyo kutoka Uganda kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya kufuatia aliyekuwepo, Beartice Kiraso, kumaliza muda wake wa kazi. Vilevile wakuu hao waliridhia pendekezo la kumuongezea mkataba wa miaka mingine mitatu, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Jean Clausde Nsengiyumva, kutoka Burundi.

Kuhusu maombi ya Sudan Kusini ya kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo, wakuu hao wamekubali mapendekezo ya baraza la mawaziri ya kuundwa kwa timu ya uhakiki itakayohusisha wataalamu watatu kutoka kila nchi mwanachama na wengine watatu kutoka katika sekretarieti ya jumuiya hiyo kwa ajili ya kuwezesha mchakato huo. Timu hiyo ya uhakiki, pamoja na mambo mengine itapitia maombi ya nchi hiyo na kuona kama yanakidhi vigezo vya mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo ili kuwa mwanachama.

Vigezo hivyo ni pamoja na masuala ya kijiografia yaani kama nchi ya Sudan Kusini inapakana au iko karibu na mojawapo ya nchi mwanachama wa jumuiya hiyo; nchi kuzingatia kanuni na misingi ya kimataifa ya demokrasia, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na mchango wa nchi katika kuimarisha ushirikiano ndani ya jumuiya.

Wakuu hao wa nchi pia walizungumzia masuala ya usalama katika kanda ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na mgogoro unaoendelea baina ya Sudan na Sudan Kusini na kuzitaka nchi hizo kurudi kwenye meza ya mazungumzo kumaliza tofauti zao.

Mkutano huo maalumu wa 10 wa wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo, ulifanyika mjini Arusha na kuhudhuriwa na marais Jakaya Kikwete (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda), Mwai Kibaki (Kenya), Paul Kagame (Rwanda), Therence Sinunguruza, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi na Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII