HABARI MPYA LEO  

AZAM YAPEWA USHINDI

By Maganga Media - Apr 27, 2012

Kamati hiyo ya ligi imeipa Azam ushindi wa mabao 3-0 kwa mujibu wa Ibara ya 31 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, timu itakayohesabika kupoteza mechi (Mtibwa Sugar) itakuwa imefungwa mabao 3-0.

Vile vile kwa mujibu wa Kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom kifungu cha 22(3-6), Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh 500,000 na kupoteza mapato yote ya mchezo huo na inatakiwa kulipa faini hiyo kabla ya mechi inayofuata.

Kamati hiyo ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pia imemuondoa mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma kwenye orodha ya waamuzi kwa kuvuruga mechi hiyo ya Azam na Mtibwa Sugar iliyochezwa Aprili 23 mwaka huu.

Pia waliokuwa waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo, Samuel Mpenzu na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha nao wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Kamati hiyo ya ligi pia imesema mwamuzi wa mechi namba 160 kati ya Moro United na Oljoro JKT, Nathaniel Lazaro wa Kilimanjaro amefungiwa miezi sita na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa kutozingatia kutunza muda kwa mujibu wa kanuni ya 26(1)(f).

Nao makamishna watatu; Abdallah Mitole wa Dar es Salaam, William Chibura (Musoma) na Omari Mawela (Mwanza) wameondolewa kwenye orodha ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kufika kwenye mechi walizopangiwa kusimamia bila taarifa.

Nayo Moro United imepigwa faini ya sh 500,000 na Kamati hiyo baada ya wachezaji wake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadirishia (dressing rooms) wakati wa mechi namba 171 kati yao na Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 8(16).

Kamati hiyo ya ligi pia imelitupa pingamizi la Villa Squad dhidi ya African Lyon, ambapo Villa walikuwa wakidai wakati wa mechi yao Lyon walitumia wachezaji wawili (Mohamed Samata na Benedict Jacob) ambao mikataba yao imemalizika, Kamati ya ligi imedai wachezaji hao wana wana leseni halali za kucheza ligi.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII