HABARI MPYA LEO  

WAZAZI WALALAMIKIA UTARATIBU WA KULIPIA ADA BENKI

By Maganga Media - Mar 14, 2012

Stesheni ya Kigoma
Na mwandishi wetu.
Wazazi wa wanafunzi  wa shule za sekondari mbalimbali mkoani Kigoma wamelalamikia suala la wanafunzi kulipa ada na michango mbalimbali kupitia benki. Wakiongea na mwandishi wetu walisema kuwa hawana nia ya kupingana na maendeleo bali kwanza wazazi wa wanafunzi hao hawajaandaliwa vizuri kuhusu mabadiliko hayo na pia wanafunzi wanatumia muda mwingi katika kupanga foleni benki ili kuweza kulipa michango yao. 

Aidha mwandishi wa habari hii aliweza kuwaona baadhi wanafunzi wakikabiliwa na adha hiyo huku wenzao wakiwa madarasani. "Baba ameenda kazini na mama anasema mambo ya benki hayajui hivyo nimelazimika kuja kulipa mwenyewe benki", aliongea mwanafunzi aliyehojiwa.

Nao baadhi ya wakuu wa shule wakizungumzia kuhusu suala hili wamasema njia ya kulipia pesa benki imewasaidia kukusanya michango na ada za wanafunzi bila kuwa na kero zilizokuwepo mwanzoni za mwanafunzi kudai hajapewa risiti na hivyo kuendelea kudaiwa. "Hiyo ni pesa mwandishi, inapopitia kwenye mikono ya watu wengi kuna upotevu au kutokuwasilishwa kwa wakati husika kutokana na hali ya kibinadamu kwa anayezipokea, tangu tumeanza kutumia mfumo huu kero zimepungua", alisema. 

Mfumo huu sio mgeni nchini na umekuwa ukitumiwa na wanafunzi wa shule za bweni hasa wanapoanza safari hivyo kumfanya mwanafunzi kusafiri na risiti tu hivyo kuondoa upotevu wa pesa. Aidha wazazi wameshauriwa kufanya taratibu za kibenki siku za Jumamosi ili siku za kazi mwanafunzi aweze kusoma bila kikwazo chochote. Naye mfanyakazi wa benki ya NMB mkoani hapa amesema kuwa ili kurahisisha zoezi hilo, wamekuwa wakiwapa mhudumu mmoja wanafunzi wanaokuwa wamevaa sare za shule ili awahudumie kwa haraka na waweze kurudi shuleni kuendelea na masomo yao. 

http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII