Ujerumani yapata Rais mpya
By Maganga Media - Mar 18, 2012
Joachim Gauck , mwenye umri wa miaka 72, mwanaharakati wa zamani kutoka iliyokuwa Ujerumani ya mashariki anatarajiwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa tatu nchini Ujerumani katika muda wa miaka miwili.
Gauck anachaguliwa baada ya kupata kuungwa mkono kutoka katika vyama vya kisiasa nchini humo, lakini mwanathiolojia huyo huenda akawa mshirika mgumu kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Merkel amemkubali Gauck kwa shingo upande kushika wadhifa huo ambao ni wa heshima tu , baada ya mshirika katika serikali yake ya mseto kujiunga na vyama vya upinzani mwezi uliopita kumuunga mkono katika hatua ya kuchukua nafasi ya Christian Wulff, aliyejiuzulu kufuatia kuhusika katika kashfa ya kupata takrima ya fedha.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (CDU) |
Tofauti na Wulff, ambaye ni mbunge wa zamani kutoka chama tawaka cha kansela Merkel cha CDU, Gauck hana mafungamano na chama chochote, Lakini anafahamika kwa kusema kile anachofikiria , kwa hali ambayo ni kama anahubiri, hata katika masuala yenye utata.
Rais aliyelazimika kujiuzulu Christian Wulff |
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la Infratest siku ya Jumamosi, asilimia 80 ya Wajerumani wanamuamini Gauck, mchungaji wa zamani wa kanisa la Lutheran na mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu. Hata hivyo theluthi mbili wamesema kuwa wanafikiria atakuwa ni rais ambaye vyama vya siasa havitajisikia kuwa katika hali ya utulivu nchini humo.
Nchini Ujerumani, rais anachaguliwa sio na wapiga kura wa kawaida lakini huchaguliwa na baraza maalum lenye wajumbe 620 kutoka bunge la Ujerumani , Bundestag na idadi kama hiyo ya wawakilishi wa majimbo 16 ya Ujerumani .Kuchaguliwa kwa Gauck ni hakika kwasababu anaungwa mkono na vyama vitatu ikiwa ni pamoja na chama tawala cha CDU na kile cha upinzani cha SPD na kijani.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII