HABARI MPYA LEO  

Mpanda kupata Chuo Kikuu cha kilimo

By Maganga Media - Mar 13, 2012

HALMASHAURI  ya  Mji  Mpanda, Mkoa  mpya  wa  Katavi,  ipo  katika  mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (Kua) kama moja ya vitega uchumi na kuboresha huduma muhimu kwa maendeleo ya jamii na uchumi.
Akizungumza kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, Kaimu Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Mji Mpanda, Nzori Kinero,  alisema katika hatua za awali,  halmashauri hiyo imekiombea chuo hicho zaidi ya Sh3 bilioni kutoka taasisi za fedha.
Kinero alisema wakipata fedha za awali zitasaidia kuanzia uanzishwaji  wa  chuo hicho ambacho kinatarajiwa kujengwa mwaka huu.

 “Hata hivyo Commecial Bank of Africa (T) Ltd, wako tayari kutoa kiasi hicho  cha fedha kwa ajili ya uanzishaji wa chuo harti kwamba dhamana ya Serikali  Kuu, Halmashauri ya Mji Mpanda ambaye ni mmiliki wa chuo nayo pia iwe  mdhamini wa pili,” alisema Kinero na kuongeza:
“Mchakato wa kupata udhamini wa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Fedha  unaendelea vizuri na uko katika hatua za mwisho.”  
Awali, Kinero alilieleza baraza hilo kuwa halmashauri imeruhusiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa namba 8 ya mwaka 1982,  lengo likiwa ni kuiwezesha kutekeleza malengo na majukumu yake makuu.
Alisema kwa kutekeleza mradi huo, halmashauri itaongeza na kuboresha  huduma za jamii na uchumi, siyo kwa wakazi wa Mpanda pekee bali Tanzania na kwamba, tayari imepata usajili wa muda na kutambuliwa na Tume ya Vyuo  Vikuu Tanzania (TCU).
Tayari suala hilo lilishajadiliwa kwenye Kamati ya Fedha na Utawala Februari 22,  mwaka huu na hatimaye juzi kufikishwa katika baraza la madiwani ambalo  limeridhia halmashauri kutoa dhamana.
Wakati huohuo, magogo 470 ya mininga ambayo yamevunwa kinyume cha  sheria na yamekamatwa maeneo mbalimbali kwenye Msitu wa Hifadhi ya Kijiji cha Inyonga, Wilaya ya Mpanda, Mkoa  mpya wa Katavi kufuatia msako  maalumu uliofanywa hivi karibuni.
Kaimu Ofisa Maliasili wa Hamshauri ya Wilaya ya Mpanda, Josephine Rupia,  ambaye pia ni Ofisa Wanyamapori, alisema kati ya magogo hayo yaliyokamatwa ni 107, yaliyosafirishwa na kuhifadhiwa mjini Mpanda, 300  yaliyosalia yapo Inyonga.
Kapufi  alisema thamani halisi ya mabao na magogo hayo haijafahamika  na kwamba, yamehifadhiwa eneo la Ofisi ya Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Mpanda mjini, yakisubiri utaratibu wa kisheria ili yauzwe kwa mnada wa  hadhara.

http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII