HABARI MPYA LEO  

Dk Kawambwa awaonya wanafunzi wadanganyifu

By Maganga Media - Mar 10, 2012

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Skukuru Kawambwa, amesema wanafunzi wa Elimu ya Juu watakaobainika kufanya udanganyifu ili wapate mikopo watashtakiwa. Akitembelea Chuo Kikuu cha Ardhi na kukutana na uongozi wa chuo na Serikali ya wanafunzi jana, Dk Kawambwa alisema pia maofisa wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu watakaobainika kushiriki udanganyifu huo watashtakiwa.
“Wanafunzi watakaodang’anya na kujipatia fedha zaidi za mikopo watashtakiwa, wakiwamo watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,”alisema.
          Pia, Dk Kawambwa aliwataka viongozi wa vyuo vya elimu ya juu kusimamia kwa karibu suala la mikopo iliyotolewa kwa wanafunzi, ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza hasa baada ya utaratibu wa kupitisha fedha za mikopo vyuoni badala ya kuzipeleka moja kwa moja kwenye akaunti za wanafunzi.“Dawati la mikopo lililoanzishwa kila chuo cha elimu ya juu litumike vizuri ili kuondoa matatizo yanayojitokeza katika kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya wanafunzi, hasa kuwasiliana na bodi ya mikopo badala ya kuwaachia wanafunzi kuwasiliana moja kwa moja,” aliagiza Dk Kawambwa.

Katika hatua nyingine, Dk Kawambwa aliwataka wanafunzi wa elimu ya juu, kujiepusha na migogoro ya aina yoyote wanapokuwa vyuoni.

“Tunataka mkitoka hapa muwe wataalamu wazuri mnaoweza kushindana katika soko la ajira, tusijenge taifa la walalamikaji na wazomeaji. Taifa letu linawategemea ninyi ili kuweza kuliletea maendeleo,” alisema Dk Kawambwa. Alisema wanafunzi watakaojiingiza katika migogoro hawatasamehewa na badala yake, watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za vyuo vyao.

Kauli hiyo ya Waziri Kawambwa kutaka uongozi wa chuo ufuatilie kero za wanafunzi bodi, ilikuja baada ya Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Ismail Mvungi, kumtaka kushughulikia kero ya ucheleweshaji mkopo. Awali, Mvungi alisema ucheleweshaji wa mikopo ya wanafunzi husababisha usumbufu kwao.Wakati huohuo, Waziri Kawambwa amezindua bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea), huku akisema bado ina changamoto zinazoikabili.

Mwenyekiti wa bodi hiyo ni Dk Naomi Katunzi, Katibu wake ni Rosemary Lulabuka ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Tea, wajumbe ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei, Profesa Siriel Masawe, Profesa Emmanuel Bavu, Vuai Khamis Juma na Muwhela Kalinga.

http://maganga-resources.blogspot.com
 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII