Walimu rudini kazini
By Mhariri - Aug 3, 2012
Chama Cha Walimu Tanzania-CWT-kimetangaza kusitisha rasmi mgomo wa walimu na hivyo kuwataka walimu wote nchini kurejea kazini mara moja kuanzia leo ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama kawaida.
Akitoa tamko la CWT kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kukiagiza Chama hicho kitoe maelekezo kwa wanachama wake kurudi kazini, Rais wa Chama hicho GRATIAN MUKOBA amesema walimu wanarudi kazini wakiwa wamekata tamaa kutokana na hukumu hiyo.
Amefafanua kuwa walimu wanaporudi kazini bila kuwa na mawazo yaliyotulia, utendaji wao utaathirika hivyo Chama kinatoa wito kwa Serikali kukutana na CWT kwa haraka ili kuendeleza majadiliano ya Madai mapya ya Walimu.
Kuhusu kulipa fidia ya hasara waliyoipata wanafunzi, Chama hicho kimesema kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hasara hiyo kwa kuwa hakina uwezo wa kufahamu hasara waliyoipata wanafunzi. Kwa mujibu wa Mwalimu MUKOBA wenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo ni mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Serikali.
Hapo jana Chama hicho kilipongeza kauli ya Rais JAKAYA KIKWETE yakusema Serikali inajali na kuthamini mchango wa Walimu nchini.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII