HABARI MPYA LEO  

Highlights za Hotuba: Mafuta yala dhahabu yote, korosho na viwanda-Zitto

By Mhariri - Aug 15, 2012

2.1 Mauzo ya Nje
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuhakikisha kuwa Akiba ya Fedha za Kigeni nchini inakuwa imara muda wote. Biashara ya nje ndio inaingiza Fedha za kigeni nchini kwa hiyo ni eneo la kutazama kwa makini na kuchukua hatua mwafaka. Taarifa ya mwenendo wa uchumi kwa mwezi Julai iliyotolewa na Benki kuu inaonyesha kuwa jumla ya mauzo ya Tanzania  nje yalikuwa dola za kimarekani 7,990.0 milioni ukilinganisha na kiasi cha dola 7,050.7 milioni kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2011 na hali hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa bei ya mauzo ya dhahabu. Hata hivyo Manunuzi yetu kutoka nje yamefikia dola za Kimarekani 12,959 milioni.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya dhahabu Nje kwa mwaka 2011 yalikuwa kiasi cha dola 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7% ya mauzo yote nje, wakati mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa viwandani yalikuwa na jumla ya dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4% ya mauzo yote ya nje. Aidha mauzo ya mazao mbalimbali kama Pamba, Katani, Korosho, Chai, Kahawa na mengineyo yalikuwa na thamani ya dola 761.1 milioni kwa kipindi hicho cha mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo imeendelea kuonyesha kuwa tuliagiza bidhaa kutoka nje zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 12,958.7.  Katika manunuzi hayo tuliyofanya mafuta peke yake yalikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 3,586.1  ambalo ni ongezeko la asilimia 60.08% ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonyesha kwamba fedha zote za kigeni zilizotokana na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani na Korosho zilitumika kuagiza mafuta pekee yake! Hali hii ni mbaya sana kwa uchumi wa Taifa letu na juhudi zote za kuongeza mauzo nje zinaliwa na uagizaji wa Mafuta ambao umepanda sana katika siku za hivi karibuni.

Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa kuanzia mwaka jana Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Umeme wa dharura ambao umepelekea matumizi makubwa ya Mafuta. Hata hivyo ieleweke kuwa Mpango mzima wa Manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya Umeme inaligharimu Taifa Fedha nyingi sana. Takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inapaswa kutumia zaidi ya shilingi 42 bilioni kila Mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya Umeme. Manunuzi yenyewe ya Mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri. Licha ya kutaka Spika aunde timu ya kuchunguza ufisadi katika manunuzi ya Mafuta na licha ya Kamati ya Bunge kutaka Uchunguzi wa kibunge kufanyika katika manunuzi haya bado hakuna hatua inayochukuliwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma PPRA kufanya uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha Umeme ambayo yanachoma bilioni 42 za Serikali kila Mwezi. PPRA hapaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna shilingi 1.4 bilioni kila siku na yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje (imports) na hivyo kupoteza fedha za kigeni hovyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ambayo ndio wizara mama ya PPRA kupitia Fungu 50, na ndio Wizara yenye kusimamia uchumi wa nchi kwa ujumla ituletee Bungeni Taarifa ya Uchunguzi utakaofanywa na PPRA kuhusu manunuzi shilingi 1.4 bilioni kila siku ya mafuta kuendesha mitambo ya kuzalisha Umeme.

CHANZO: http://zittokabwe.wordpress.com/2012/08/15/highlights-za-hotuba-mafuta-yala-dhahabu-yote-korosho-na-viwanda-zitto/

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII