Taarifa ya Serikali juu ya ajali ya meli
By Unknown - Jul 20, 2012
WIZARA YA HABARI UTAMADUNI UTALII NA MICHEZO
Tel: 0255 24 2237325/0255 24 223 7313
Maelezo
Fax: 0255 24 2237314
E-mail:habarimaelezo@yahoo.co.uk, maelezozanzibar@zanlink.com
maelezozanzibar@hotmail.com, maelezozanzibar@gmail.com
TAARIFA YA SMZ KUHUSU AJALI YA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOLEWA
USIKU HUU JULAI 19,2012
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa taarifa usiku huu ikieleza idadi ya watu waliopatikana
wakiwa hai ni 146 na kupata maiti 62.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari usiku leo,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Ali Juma Shamuhuna alisema taarifa hiyo ndio sahihi na kuwataka wananchi kutoamini taarifa
zinazotolewa na watu wengine zaidi ya Serikali.
Waziri Shamuhuna alisema kwamba maiti 62 walipatikana ambao kati ya maiti hizo watoto ni
9 na kuna raia mmoja wa kike wa kigeni ambaye hakuweza kutambulika Uraia wake,lakini
umeonekana picha yake moja ndogo ya hati ya kusafiria.
Waziri Shamuhuna alisema meli hiyo ilibeba jumla ya abiria 290 kati ya hao watu wazima 250,
watoto wadogo 31 na mabaharia 9.
Waziri huyo aliwataka wananchi katika sehemu mbalimbali hasa katika vijiji vilivyo
kandokando ya bahari watakapoona maiti au mtu akiwa hai ambaye wanadhani ni wa ajali ya
Meli ya Skagit.
Aidha, Waziri Shamuhuna alisema kwamba kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambao
watakuwa na wasiwasi wa kutowaona ndugu na jamaa zao amewataka kufika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata taarifa zaidi au kuripoti habari za kupotelewa kwa
ndugu au jamaa zao.
Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo aliwataka wananchi kufika kwa Masheha wao kutoa
taarifa kama hizo.
Serikali imewashukuru makampuni binafsi za usafiri baharini kwa msaada wao na wasisite kutoa
msaada katika kazi inayoendelea ya kutafuta watu au maiti wengine katika eneo la tukio.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali wa maili sita
kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam
ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake
nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka
2009.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
ZANZIBAR, TANZANIA
JULAI 19,2012
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII