HABARI MPYA LEO  

Kiswahili chombo cha kupitishia maadili!

By Unknown - Jul 20, 2012

Na Gadi Solomon
MAADILI ya jamii hapa nchini yamekuwa yakitafutiwa njia mbalimbali ili yaweze kuimarika kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Awali, uhusiano mzuri, mshikamano na uzalendo miongoni mwa wanajamii vilikuwa vimeimalika ukilinganisha na hali inavyoonekana hivi sasa.
Pengine, hali hiyo imesababisha Serikali kurudisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha maadili ya jamii na uzalendo kwa wanajamii.
Miaka ya hivi karibuni suala la mmomonyoko wa maadili limekuwa likipigiwa kelele kwa kiasi kikubwa, kutokana na mambo mbalimbali ambayo yanaendelea katika jamii ikiwamo watu kujichukulia sheria mikononi jambo ambalo ni uvunjaji wa maadili ya jamii licha ya jamii licha ya wanajamii kuusiwa kuacha tabia hiyo, tena kwa lugha wanayoielewa ya Kiswahili.
Matukio mbalimbali ambayo yamelitikisa taifa miaka ya hivi karibuni kama vile mauaji ya albino, kujichukulia sheria mikononi kuwauwa watuhumiwa pamoja na mauaji ya vikongwe.
Yote haya yanaweza kuwa ishara kuwa jamii imepungukiwa maadili.
Hayo yanapotendeka tunacho chombo muhimu ya kusaidia katika jamii kupata ujumbe kwa namna mbalimbali kutoka kwa viongozi wao ambacho ni lugha.
Tunayo lugha ya taifa, yaani Kiswahili ambayo haipewi mkazo kwa asilimia kubwa kutokana na watu kuipuuzia. Iwapo watu wanazarau lugha yao watawezaji kusikiliza yale wanayoagizwa kwa kutumia lugha hiyo?
Ndiyo maana labda wakati mwingine watu na viongozi wanadiriki kutumia lugha za kigeni katika kuelezea msisitizo katika jambo fulani akiamini ujumbe na hisia zake zinaweza kufika kwa walengwa.
Jambo la kushangaza ni kwamba lugha ya taifa imekuwa haipewi msukumo katika mambo mbalimbali, ambayo watalaamu na walimu wa Kiswahili wamekuwa wakitoa mapendekezo yao.
Upo umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili katika ujenzi wa maadili ya kijamii. Katika historia ya ukuaji wa lugha hii kabla ya uhuru na baada ya uhuru Kiswahili kilikua kwa njia ya mafundisho ya dini makanisani au misikitini.
Hivi sasa licha ya taasisi hizo muhimu za dini ambazo ndiyo zilichukua nafasi pia katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili, kwa hivi sasa pia ndiyo taasisi ambazo zinaweza kujenga maadili ya jamii kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika mawaidha na ibada.
Ujenzi wa maadili kupitia taasisi hizi za dini sehemu muhimu, kutokana na kuwa na jukumu la kurekebisha mienendo ya watu ambao miongoni mwa hao wapo viongozi serikalini.
Ni kupitia lugha ya Kiswahili maadili ya jamiii hayo yanayotolewa yakizingatiwa, yanaweza kuharakisha maendeleo katika taifa letu.
Mathalan hali halisi ilivyo sasa, vijana wanapata elimu ya dunia kwa lugha za kigeni yakiwamo mambo mbalimbali kama maadili na uzalendo.
Ukweli ni kwamba, mambo kama hayo muhimu yanaweza kueleweka vyema zaidi, iwapo watu watapata maarifa hayo kwa lugha ya taifa inayoeleweka na wengi.
Ilifika wakati baadhi ya wanajamii hao hao waliopata maarifa ya elimu ya dunia na kumudu kugha za kigeni, walikuwa wakidharau wazazi wao wasiojua lugha hizo mara nyingine kujitenga na na jamii, jambo ambalo si sahihi.
Bado kumekuwapo na maswali mengi kwa nini maadili kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakiporomoka kwa jamii. Leo hii mtoto unamweleza jambo anaitikia lakini hatekelezi.
Pia, hivi karibuni Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala alieleza bungeni mjini Dodoma kuwa, haiwezekani lugha ya Kiswahili ikakubaliwa kutumika katika mahakama zetu pendekezo ambalo pia lilishawahi kutolewa na wajumbe wa APRM walipokuwa katika tathmini za utawala bora kwa nchi za Afrika walipozuru hapa nchini mwanzoni mwa mwaka huu.
Swali la kujiuliza ni je, iweje mataifa mengine yameweza kutumia lugha zao na sisi wenye lugha inayokubalika ulimwenguni tumekuwa tunasita kuwa na uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili? Waswahili wana msemo wake kwamba kila jambo na wakati wake, yumkini zama za Kiswahili kukubalika na watawala hazijafika kutokana na umuhimu mdogo unaopewa na watendaji wake.
Lugha za taifa ulimwenguni kote hutumika katika maeneo mbalimbali kwa nchi nyingi ulimwenguni na lugha hizo ndiyo zinazotumika katika kupashana habari na suala la ujenzi wa maadili ya jamii husika.
Jambo la kushangaza ni namna mataifa ya kigeni ambavyo yamekuwa yakikipigania Kiswahili ikiwemo kuweka mikakati mbalimbali kuhusiana na kuendeleza lugha za Afrika, hata kuanzisha Idara za Lugha za Kiafrika katika vyuo vyao huko ughaibuni.
Aidha, tunazo Mbuga za Serengeti na nyinginezo nyingi, Mlima Kilimanjaro lakini tumeshindwa kuandaa santuri za sauti kwa Kiswahili ili kuelezea vivutio vyetu na kuviuza.
Vitu hivyo vimekuwa vikifanywa na majirani zetu na raia wa kigeni kwa maufaa yao jambo ambalo tunao uwezo wa kukitumia Kiswahili kuelezea jamii yetu mambo mbalimbali mazuri yanayoendelea.
Hii haimanishi shughuli mbalimbali za Kiswahili hazifanyiki, ukweli ni kwamba hazifanyiki kwa kiwango kinachoendana na maendeleo na mafanikio ya lugha ya Kiswahili ulimwenguni.
Itakumbukwa nyimbo mbalimbali za akari wetu wakiwa vitani miaka ya sabini ziliimbwa kwa lugha ya Kiswahili katika kuwapa hamasa na kuwajenga kuwa wazalendo.
Ni vyema tukatumia Kiswahili katika ujenzi wa maadili ya jamii yetu badala ya kukazania kupitisha ujumbe kwa lugha ambazo si watu wengi wanazielewa. Hivyo maadili ya taifa hili yanaweza kujengwa pia kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika taifa letu la Tanzania.
*Mwandishi ni mhakiki wa lugha wa gazeti la Mwananchi. Simu: 0712127912

PATA UNACHOKITAKA KWA WAKATI MUAFAKA

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII