HABARI MPYA LEO  

Simbachawene: Sijafumaniwa

By Emmanuel Maganga - Jun 25, 2012

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, ameibuka na kukanusha vikali uvumi ulioenea jana kuwa amefumaniwa na mke wa mtu mjini Singida usiku wa kuamkia jana na kujeruhiwa mkono kwa kisu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Karatu jana jioni, Simbachawene ambaye pia ni Mbunge Kibakwe (CCM) mkoani Dodoma, alisema habari hizo ni uongo na kudai kuwa zimeenezwa na baadhi ya wabunge wa Chadema aliokutana nao mjini Singida jana wakati akiwa njiani kwenda msibani Karatu.

Alisema kuwa katika hoteli aliyofikia, kuna mtu alifumaniwa akiwa na mke wa askari na kufafanua kuwa watu walizua jambo hilo kwa kuwa naye alilala katika hoteli hiyo.

Aliwataja watu wanaodaiwa kueneza uvumi huo hizo kuwa ni wanachama wanane wa Chadema akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu kupitia chama hicho, Christina Lissu. “Baada ya kufika Singida nilikwenda katika baa moja na kuwakuta wabunge wa Chadema na baadhi ya wanachama, nilipata kinywaji na kurudi hotelini kulala,” alisema Simbachawene.

Huku akivua shati kuwaonesha waandishi wa habari kwamba hakukatwa mapanga mikononi kama ilivyodaiwa, alisema kuwa alipoamka asubuhi ndipo alianza kusikia habari kuwa amefumaniwa na mke wa mtu.

Awali taarifa kutoka Singida zilizowekwa pia kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa Naibu Waziri huyo alikumbwa na mkasa huo jana alfajiri. Tukio hilo ambalo inaelezwa kuwa lilitoka majira ya saa kumi, baada ya taarifa hizo kumfikia mwenye mke, ilimlazimu mmiliki wa hoteli hiyo kutoa taarifa Polisi ili kuzuia maafa zaidi

Uvumi huo ulidai kuwa baada ya taarifa hizo, iliwalazimu askari Polisi kwenda katika hoteli hiyo ili kumuokoa Simbachawene, ambaye tayari alikuwa amejeruhiwa mkono kwa sime na askari huyo mwenye mke.

Mara baada ya purukushani hizo katika eneo hilo Naibu Waziri huyo alidaiwa kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi mkoani Singida, ambapo ilidaiwa kuwa katika maelezo yake aliandika jina la Josephat Joseph badala ya kutumia jina lake halisi.

Hata hivyo, Mbunge Christina Lissu, alisema anashangazwa na taarifa za yeye kuhusishwa kueneza uvumi huo.

Alisema walikutana na Naibu Waziri huyo, katika hoteli hiyo, wakiwa wanatoka mkoani Tabora katika kesi na wabunge wa Chadema, Conchesta Rwamlaza, Philipa Muturano na John Mrema ambaye ni Mkurugenze wa Bunge na Halmashauri ya chama hicho.

CHANZO: Mwananchi Jumapili

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII