HABARI MPYA LEO  

Shambulio la kigaidi nchini Kenya

By Unknown - Jun 25, 2012


Shambulio la kigaidi nchini Kenya

Mtu mmoja ameuwawa katika mlipuko uliotokea katika baa moja iliyoko viungani mwa mji wa Mombasa nchini Kenya.Polisi wamesema zaidi ya watu wanane wamejeruhiwa kufuatia shambulio hilo lililotokea saa nne, Jumapili usiku.Shambulio hilo limejiri siku moja baada ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya kuonya kuwa ''kulikuwa na tisho la kutokea shambulio la kigaidi'' katika eneo hilo.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo amesema kuwa , wakati mlipuko huo ulipotokea, baa hiyo ilikuwa na wateja wengi waliokuwa wakitizama mechi ya robo fainali kati ya Uingereza na Italia, katika michuano ya kombe la taifa bingwa bara Ulaya.

Mapema wiki hii, maafisa wa polisi wa Kenya waliwakamata raia wawili wa Iran waliotuhumiwa kuhusika na mtandao wa kigaidi unaopanga kutekeleza mashambulizi mjini Mombasa. Siku ya Jumamosi, polisi katika mji mkuu Nairobi, walisema kuwa walipata vifaa vinavyo shukiwa kutumika katika kutengeneza bomu.

''Taarifa tulizopata ni kwamba kifaa hicho ambacho tunashuku ni gruneti, kilirushwa na mtu mmoja aliyekuwa akiburudika kwenye baa hiyo. Hatukuweza kumnasa mtu huyo lakini tunaendelea na uchunguzi,'' Adoli aliambia kipindi cha Amka na BBC.

Mbali na Marekani, ubalozi wa Ufaransa mjini Nairobi pia umeonya raia wake '' kuwa waangalifu'' wakiwa katika mji huo wa Mombasa. Marekani iliwatahadharisha raia wake kutozuru Mombasa hadi Julai mosi.

Mwezi Mei, mtu mmoja aliuwawa wakati kilipuzi kiliporushwa ndani ya mkahawa mmoja mjini humo. Kumekuwa na msururu wa mashambulizi ya gurunedi tangu Kenya ilipopelekwa wanajeshi wake nchini Somalia kuwasaka wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al- Shabab, mwezi Oktoba mwaka jana.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII