HABARI MPYA LEO  

Mtei amtetea Mnyika

By Unknown - Jun 21, 2012


MWASISI wa Chadema, Edwin Mtei amemtetea Mbunge wa Ubungo, John Myika kuwa alikuwa sahihi kusema kwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, kwa kuwa kuna matukio mengi yaliyohitaji uamuzi wake na hakuutoa kwa wakati.

Pia Mtei amelaumu Kanuni za Bunge zilizomwezesha Naibu Spika, Job Ndugai kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge mbunge huyo.

Juzi, Mnyika alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya kukukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’.

Akitetea kauli hiyo, Mtei alirejea baadhi ya matukio aliyodai yanaonyesha udhaifu huo, ukiwamo uamuzi ya Rais Kikwete juu ya hatua za kuwachukulia walioiba fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mtei alifafanua kwamba, kitendo cha Rais Kikwete kuwataka wezi hao warudishe fedha walizoiba badala ya kuwakamata, kinadhihirisha udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo. “Rais Kikwete ana udhaifu wa kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wanahujumu taifa kwa ufisadi…udhaifu wa Rais ni kama kutowadhibiti wezi wa fedha zetu kama fedha za EPA. Aliwaambia wezi warudishe fedha, badala ya kuwatia ndani wanabaki wanatamba kwa kuiba fedha zetu,” alisisitiza Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu. Alisema kibaya zaidi ni kwamba, nchi inayumba kutokana na uongozi mbovu kuanzia ngazi ya urais hadi chini, kwa kuwa tunaongozwa na watu wasiojua na kuisimamia Katiba.

Akitoa maoni yake juu ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu, Mtei alisema Bajeti hiyo haina jipya kwa kuwa haishughulikii matatizo na kero za wananchi pamoja na kukabilina na mfumuko wa bei unaolikabili taifa. Kuhusu suala la deni la Taifa linalofikia Sh20.2 trilioni, alisema nchi ipo njia panda, hali ambayo ni hatari kwa kuwa ni mzigo kwa taifa na linazidi kuongezeka kila mwaka.

Mwanasiasa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa kwanza wa Chadema, aliponda vitendo vya Serikali kukopa fedha kila mara kwenye mabenki ya kibiashara nchini, na kuomba kwa wahisani.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII