HABARI MPYA LEO  

Lowasa: Hawaniwezi na kuninyima usingizi!

By Maganga Media - Jun 4, 2012

ATAMBA, MAADUI ZAKE HAWATAMNYIMA USINGIZI

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amewapiga vijembe aliowaita maadui zake kisiasa wanaomchafua katika majukwaa mbalimbali akisema kuwa, hawamuwezi na hawamnyimi usingizi.

Lowassa akitambia maadui zake, kambi yake nayo imezidi kujizatiti baada ya mshirika wake kisiasa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amefanikiwa kukalia kiti cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi hivyo kuzidi kuongeza nguvu kwenye bungeni.

Jana, akiwa mkoani Arusha katika harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Elaira, Lowassa alitumia sehemu ya muda wake kuwapiga vijembe maadui zake pasipo kuwataja majina akisema kamwe hawamnyimi usingizi.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alitoa kauli hiyo, baada ya Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer kumtaka aendelee kufanya kazi ya Mungu licha ya baadhi ya watu kumkatisha tamaa.

Akizungumzia kauli ya Askofu Laizer, Lowasa alisema mahasimu wake kisiasa wamekuwa wakimsema kupitia vyombo mbalimbali vya habari, lakini akatamba kwamba juhudi hizo hazitaweza kufua dafu kwake kwani kelele zao hazimnyimi usingizi.

“Wanaonisema kwenye magazeti wala hawanisumbui, nasema hawaninyimi usingizi kwa kuwa mimi namtegemea yule anitiaye nguvu daima,” alisema Lowasa, kitendo kilichosababisha kushangiliwa na waumini waliohudhuria kanisani hapo.

Aliongeza kuwa yeye daima humtegemea Mungu amtiaye nguvu na kamwe hawezi kushindwa kulala usingizi kwa kusikiliza kelele zao za mara kwa mara.

“Nakushukuru Baba Askofu kwa kunijibia, wale wote wanaonisemasema kwenye magazeti wala hawanisumbui na wala hawaninyimi usingizi,” alisema Lowasa.

Alisema kwamba yeye ataendelea kumtumikia Mwenyezi Mungu ambaye amtiaye nguvu siku zote bila kujali maneno ya mahasimu wake wa kisiasa.
Kabla ya kuendesha harambee hiyo, Lowasa aliwaongoza waumini wa kanisa hilo kwa nyimbo zilizopo kwenye Kitabu cha Tenzi za Rohoni na kuibua shangwe kanisani hapo.
 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII