HABARI MPYA LEO  

Kashfa mgodi wa Kiwila

By Unknown - Jun 24, 2012


Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono

LICHA ya kusababisha hasara ya Sh61 bilioni, mgodi wa makaa ya mawe Kiwira uliopo mkoani Mbeya umetengewa tena kiasi cha Sh40 bilioni katika bajeti ya Serikali ya 2012/2013 iliyopitishwa jana na Bunge mjini Dodoma.Mgodi wa Kiwira ukijulikana kwa jina la Kiwira Coal & Power Limited (KCPL) ni kampuni iliyokuwa ikiundwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Tan Power Resources (TPR) ikiwa na malengo ya kufufua uendeshaji wa mgodi huo na kuuwezesha kuzalisha umeme ambao ulitarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Licha ya kwamba TPR walikuwa wabia katika ulimiki wa mgodi huo kwa kuwa na asilimia 70 ya hisa na Serikali ikiwa asilimia 30, pia wao ndio waliochukua jukumu la uendeshaji wake kinyume cha makubaliano kwamba wangetakiwa kutafuta manejimenti nyingine.

Taarifa za Serikali zinaonyesha kuwa mgodi huo chini ya menejimenti ya Kampuni ya Tan Power Resources Ltd hadi kufikia Desemba 31, 2010 umelimbikiza hasara ya zaidi Sh61 bilioni wakati madeni yake (liabilities) yanafikia Sh56 bilioni.

Kulingana na ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Hesabu ya PKF, madeni hayo yanatokana na mikopo kutoka benki na taasisi za fedha ambazo jumla yake ni Sh32.19 bilioni kutoka Benki ya CRDB inayodai kiasi cha Sh4.65 bilioni, Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) Sh11.09 bilioni na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sh16.5 bilioni.

Kadhalika, taarifa hizo za hesabu, zinathibitisha kwamba Sh23.81 bilioni ni madeni ya yanayohusiana na wafanyakazi na wadai wengine.

Kutokana na hali hiyo, nyaraka mbalimbali ambazo gazeti la Mwananchi limeziona, zinathibitisha kuwa Serikali ilishauriwa na timu ya wataalamu kutoilipa kampuni hiyo kiasi chochote baada ya kufanyika kwa uamuzi wa kurejeshwa kwake serikalini baada ya kushindwa kutekeleza kazi zake.

Uamuzi wa kurejeshwa kwa Serikalini ulitangazwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja Julai 23, 2009 baada ya kuwapo shinikizo kutoka kwa wabunge kadhaa hasa kutoka mkoani Mbeya ambao walidai kwamba imeshindwa kutimiza sababu za kuwapo kwake.

Kabla ya kutangazwa rasmi kwa uamuzi huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliliambia Bunge kwamba Serikali iliamua kufanya mazungumzo na TPR ili kurejesha hisa zake serikalini kama moja ya hatua za kuepusha kutajwa kila mara jina la Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Mkapa na aliyekuwa Waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona ndio wamiliki wa kampuni ya TPR, hivyo tuhuma nyingi zilielekezwa kwao kwamba walijiuzia mali ya umma wakiwa viongozi wa umma.

Hadi uamuzi wa kuurejesha Serikali ulipofanyika, KCPL ilikuwa haijaweza kujiendesha hivyo kushindwa kutimiza malengo yake ya kuwezesha nchi kunufaika na uzalishaji wa umeme kama ilivyokuwa imetarajiwa awali, licha ya kupewa mkopo kwa dhamana ya Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Miongoni mwa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona ni barua kutoka Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) kwenda kwa uongozi wa TPR ya Novemba 18, 2011 ambayo sehemu yake inasomeka:

“Imethibitika kwamba Kampuni ya KCPL imekuwa ikijiendesha kwa hasara kwa miaka yote chini ya uongozi wa TPR. Mali (asset book value) za KCPL zilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 19…nakisi ya mtaji (capital deficit) ya shilingi bilioni 37, na hivyo kufanya kampuni hiyo kuwa mufilisi,”inaeleza sehemu ya waraka huo wa CHC.

Kadhalika sehemu ya taarifa ya watalaamu wa CHC iliyotumwa Serikali ambayo pia gazeti hili limeiona inasomeka kuwa: “Utendaji wa KCPL tangu ubinafsishwe umekuwa hauendani na matarajio Serikali kutokana na kampuni hiyo kushindwa kuendeleza mradi wa makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme wa Kiwira kwa wakati uliopangwa. Aidha, KCPL ilishindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao ya miezi 15, kiasi cha takribani Sh2bilioni ”.

Kutokana na hali hiyo kiasi cha Sh40 bilioni kilichotengwa na Serikali ndicho kilichozua mvutano bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ambapo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrodi Mkono alihoji sababu za kupelekwa fedha hizo hali mgodi huo ukiwa umeishaisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo jana alisema hawezi kujibu hoja ya Mkono kwa maelezo kwamba Mbunge huyo ana maslahi katika mgogoro huo kutokana na kuwa mwakilishi wa Kampuni moja nchini Dubai.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII