HABARI MPYA LEO  

Bajeti ya Ulinzi yazuiwa!

By Maganga Media - Jun 8, 2012

KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa imeikataa bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kutokana na kutotenga fedha za mafunzo ya JKT, kama ilivyokuwa imeelekezwa na Serikali.

Uamuzi wa kamati hiyo umekuja siku chache baada ya kumtikisa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kutokana na kuchelewa kufikisha vitabu vya bajeti mbele ya kamati wala kuweka mchanganuo wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, zilisema wizara hiyo ilishindwa kutenga fedha hizo, ndipo kamati hiyo ilipoamuru ikarekebishe.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, vilisema uamuzi huo wa kamati uliotolewa na mwenyekiti Lowassa, ulifanyika mbele ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.

Pia, katika kikao hicho alikwepo Mkuu Mpya wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Samwel Ndomba pamoja na maofisa wengine waandamizi wa JWTZ na JKT.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII