HABARI MPYA LEO  

Shibuda aendelea kumuomba Kikwete awe meneja wake wa kampeni

By Maganga Media - May 25, 2012

MBUNGE wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda jana alirudia kauli yake ya kumuomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake wa kampeni wakati atakapojitosa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.Shibuda alifanya hivyo mbele ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta.

Kauli hiyo imekuja wakati Shibuda akiwa ameiligawa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) baada ya mwenyekiti wake, John Heche kupingana hadharani na makamu wake, Juliana Shonza kuhusu msimamo wa baraza hilo dhidi ya hatua ya mbunge huyo  kutangaza nia ya kuwania urais, akiwa  ndani ya kikao cha Nec ya CCM.

Siku mbili baadaye Shibuda aliibuka tena na kumshukia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kuwa ndiye anayewatumia vijana hao kumhujumu, kauli ambayo ilipingwa vikali na Dk Slaa.

Lakini,  jana akiwa katika semina ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki iliyowahusisha pia wenyeviti wa kamati zote za kudumu za Bunge wakiwemo wa Kamati ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Shibuda alirudia kauli yake  na kuwafanya washiriki wa semina hiyo kuangua kicheko.

“Mimi naitwa John Shibuda ni Mbunge wa Maswa Mashariki na Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, pia ninayetaka Rais Kikwete awe kampeni meneja wangu katika kampeni za mwaka 2015,” alisema wakati akijitambulisha.

Kauli hiyo ilizua zogo kwa baadhi ya washiriki wa semina hiyo ambao walianza kumpigia makofi huku Spika Makinda na Sitta wakiangua kicheko.

Shibuda juzi aliliambia Mwananchi kuwa yuko tayari kwa lolote na wakati wowote tena kwa asilimia 100 kutokana na kauli hiyo aliyoitolea katika kikao cha CCM.

Alisema kitendo cha Dk Slaa kutozungumzia shutuma zinazotolewa na vijana hao wa Chadema dhidi yake (Shibuda) kinampa fursa ya kuamini kwamba vigogo wa chama hicho wako nyuma yao.

Alimtaka Dk Slaa aeleze hadharani uovu wake huo ili Watanzania wafahamu ukweli kuhusu sakata hilo.

Akizungumza katika semina hiyo, Shibuda aliwataka wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kuzingatia mambo ya msingi kwa maslahi ya taifa.Pia aliwataka kuwa makini katika masuala ya ardhi na kutokubali kutumiwa.

“Siku zote penye uzia penyeza rupia, kuna tetesi kuwa rupia ilipitishwa kwa wabunge wa Bunge la Afrika Masharii, kwa hiyo kuweni makini, msikubali kutumika” alisema Shibuda.

Mwenyekiti wa wabunge hao, Alhaj Adam Kimbisa aliwapongeza waandaaji wa semina hiyo na kuahidi kuwa wataiwakilisha nchi katika bunge hilo kwa nguvu moja na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII