Odinga: Mudavadi huru kuondoka ODM
By Maganga Media - May 3, 2012

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na mwenzake wa Israel Benjamin Netanyau
Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amejibu hatua ya naibu wake Musalia Mudavadi kukihama chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kusema alikuwa huru kuchukua uamuzi wake.
Akizungumza na BBC mjini London, Odinga amesema kama kiongozi anayetetea demokrasia, hawezi kushtumu uamuzi wa naibu wake ambaye amejiuzulu pia kama waziri wa serikali za mitaa.
Aidha Odinga ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha ODM amesema ataachia baraza kuu la chama kuamua ikiwa itamuondoa kwenye chama Mudavadi na hivyo kupoteza kiti chake cha ubunge hatua ambayo huenda ikamfanya Naibu Waziri Mkuu kurudi kwenye uchaguzi katika jimbo lake la Sabatia, Magharibi mwa Kenya.
Tofauti kati ya Musalia Mudavadi na Raila Odinga zilichochewa na kanuni za uteuzi wa mgombea wa Urais wa ODM ambapo wanaomuunga mkono Mudavadi ulilalamika kuwa washirika wa Waziri Mkuu walipenyeza vipengele vinavyomzuia Naibu Waziri Mkuu kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.
ODM imekumbwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa wanasiasa wake ambapo tayari aliyekua naibu kiongozi wa chama hicho William Ruto alikihama chama na kufuatwa na wabunge waliomuunga mkono. Nchini Kenya wabunge wamekuwa wakihama hama vyama ambavyo viliwafadhili kuingia bungeni bila kuwasilisha waraka wa kuachia ubunge kama inavyotakiwa kisheria.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII