HABARI MPYA LEO  

MTIBWA WAIZAWADIA UBINGWA SIMBA

By Maganga Media - May 5, 2012

Mashabiki wa Simba,wakishangilia baada ya Mtibwa Sugar kuifunga Azam 2-1

MTIBWA Sugar imeikabidhi rasmi ubingwa Simba baada ya kuichapa Azam kwa mabao 2-1 katika mchezo ulioamriwa kurudiwa na Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi uliofanyika kwenye  Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulirudiwa jana baada ya ule wa kwanza kufutwa baada ya Mtibwa kuelezwa kutia mpira kwapani  na mpira kuvunjika katika dakika ya 88.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Ligi ilitoa pointi tatu na mabao tatu kwa Azam,  lakini baadaye African Lyon ilikata rufaa ya kutaka Mtibwa Sugar ishushwe daraja kwa kitendo cha kugomea mechi.

Hata hivyo, Kamati ya Nidhamu chini ya mwenyekiti wake Alfred Tibagaina ilitoa agizo la kurudiwa kwa mchezo huo , pamoja na kusogeza mbele mechi zote za mwisho hadi kesho.

Mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa kila kipindi na Awadh Issa aliyefunga kwa mpira wa kona dakika ya 25, na Juma Abdul kwa mpira wa adhabu (59) kabla ya John Boko kuifuta machozi Azam dakika 69.

Ushindi huo wa Mtibwa ni msaada kwa Simba kuwapa ubingwa kwa msimu huu huku wakiwa na mechi moja mkononi dhidi ya watani wao Yanga kesho kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba ina pointi 59 wakati Azam inabaki nafasi ya pili ikiwa na pointi zake 53. Itafunga dimba kwa kuivaa Kagera Sugar hiyo kesho kwenye Uwanja wa Chamazi.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII