Jalada la Mkulo latua TAKUKURU
By Maganga Media - May 23, 2012
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah jana alikuwa akichambua majalada ya baadhi ya mawaziri waliong’olewa baada ya wizara zao kutajwa kuhusika na ufisadi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).Tayari Dk Hoseah alikwishatangaza kwamba Takukuru imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma za mawaziri hao kabla hata ya Rais Jakaya Kikwete hajawang’oa katika mabadiliko yake ya Baraza la Mawaziri aliyofanya mapema mwezi huu huku Ikulu nayo ikiagiza uchunguzi kwa watendaji wa wizara husika.
Alisema jana hiyo alikuwa akipitia tuhuma za Mkulo kuhusu na uuzaji wa Kiwanja Namba 10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MTeL).
Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya kuchunguzwa, Mkulo alisema anachojua ni kwamba uchunguzi au mahojiano ya Takukuru na mawaziri ni wa kimaadili na ni jambo la siri. “Huwezi kusimama sokoni Kariakoo kwenye watu wengi na kutangaza kwamba tunamchunguza au tunamhoji Mkulo ni kwenda kinyume na maadili ya Takukuru,” alisema Mkulo.
Dk Hoseah alisema uchunguzi unaoendelea hivi sasa siyo kwa mawaziri hao pekee, bali unagusa pia baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali ambao wamehusishwa kwa namna moja au nyingine kwenye Ripoti ya CAG hivyo kusababisha kuwajibishwa kwa mawaziri. Alisema ripoti zilizopo kwenye ofisi yake ni za viongozi mbalimbali ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII