HABARI MPYA LEO  

Kesi za Uchaguzi kuisha kabla ya Mei 4

By Maganga Media - Apr 17, 2012



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman
Kesi nane kati ya 44 zilizofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga matokeo ya ubunge baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 zitaamuliwa kabla ya Mei 4, mwaka huu. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa majaji wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).  

Jaji Othman alisema baada ya kumalizika uchaguzi huo mwaka 2010, kesi 44 zilifunguliwa na wagombea walioshindwa katika majimbo mbalimbali na kwamba kati hizo baadhi zilifika mwisho na kutolewa hukumu, nyingine zilifutwa na zilizobaki nane ndizo zinazotarajiwa kufika mwisho na kutolewa hukumu kabla ya Mei 4, mwaka huu.  

Miongoni mwa kesi za kupinga matokeo zilizovuta hisia za watu wengi ni pamoja na ya kupinga matokeo ya Jimbo la Arusha Mjini, ambapo Aprili 5, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitengua ubunge wa Godbless Lema kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).  

Baadhi ya kesi ambazo hukumu zake zinatarajiwa kutolewa kabla ya Mei 4, mwaka huu, ni pamoja na ile ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mbunge wa Segerea, Dk. Kakongoro Mahanga.  
Nyingine ni za kupinga ushindi wa Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu (Chadema); ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opurukwa na kesi dhidi ya Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Agripina Buyogela; kesi dhidi ya Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya na kesi dhidi ya Mbunge wa Biharamulo Magharibi (Chadema), Dk. Antony Mbasa.  

Akizungumzia kesi katika mahakama mbalimbali nchini, Jaji Othman, alisema kasi ya usikilizwaji wake imeongezeka baada ya kuanzisha mfuko maalum kwa ajili kazi hiyo.  Alisema Sh. bilioni 20 zilitarajiwa kuingizwa katika mfuko huo kutoka serikalini na kwa wadau wengine ambapo kwa sasa wamepata Sh. bilioni 10.  

Hata hivyo, alisema fedha hizo licha ya kutotimia, lakini zimesaidia uharakishwaji wa kesi hususan katika mahakama za mwanzo na wilaya.  Alifafanua kuwa, awali kesi nyingi zilikwama kutokana na uhaba wa fedha kwa ajili ya kusafirisha mashahidi, kulipia posho za wazee wa mahakama na gharama zingine za uendeshaji. 

SOURCE: NIPASHE Tar 17.4.2012

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII