HABARI MPYA LEO  

Bayern Vs Chelsea Fainali

By Maganga Media - Apr 26, 2012


Bayern

Real Madrid ikichezea uwanja wa nyumbani wa Bernabeu Jumatano jioni, ilishindwa kuishinda Bayern Munich ya Ujerumani, ambao hatimaye walipata ushindi wa magoli 3-1 kupitia mikwaju ya penalti, wakati timu hizo zilipokutana katika mechi yao ya pili ya nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.
Bayern Munich ya Ujerumani, ikichezea uwanja wake wa nyumbani, sasa itaipokea Chelsea ya Uingereza katika fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.

Real ilikuwa imeachwa nyuma kwa bao moja katika mechi ya kwanza ya nusu fainali, mechi iliyokwisha kwa Bayern kushinda 2-1, lakini magoli mawili ya Christiano Ronaldo, la kwanza likiwa la penalti katika dakika ya 6, na la pili akiutambariza mpira wavuni dakika ya 14, yaliwapa mashabiki wa Real matumaini ya kufuzu kuingia fainali.

Lakini Arjen Robben alikitia kitumbua cha Real mchanga, wakati naye alipofanikiwa kutandika mkwaju wa penalti hadi wavuni katika dakika ya 27.
Schweinsteiger
Kukosekana kwa mabao zaidi katika muda wa kawaida wa dakika tisini, na hata baada ya dakika thelathini za ziada, kulimaanisha mikwaju ya penalti, na Bastian Schweinsteiger hakushindwa kuielekeza timu yake ya Bayern kwa fainali ya uwanja wa nyumbani.

Kipa Manuel Neuer alifanya juhudi kubwa, akizuia mikwaju miwili ya Real; ya Ronaldo na Kaka, huku Mario Gomez na David Alaba wakiendelea kuifungia Bayern. Hii ilikuwa ni mara ya pili pia kwa Ronaldo kukosa kufunga mkwaju wa penalti katika mechi za klabu bingwa, wakati alipokuwa akiichezea Manchester United, na katika fainali dhidi ya Chelsea mwaka 2008.

Matumaini ya meneja wa Real Madrid, Jose Mourinho, kupata ushindi wa ligi ya klabu bingwa akiiongoza klabu ya tatu kupata kombe hilo la Ulaya, inaelekea itabidi asubiri na kuwa na matumaini ya kufanikiwa wakati mwingine. Ni pigo kubwa kwa Mourinho, ambaye baada ya kuishinda Barcelona katika mechi ya Jumamosi, na akiwa na matumaini ya kuongoza katika ligi ya Uhispania, alikuwa na matumaini ya kuiongoza Real hadi fainali.

Ni klabu ya Chelsea tu ndio ilimshinda Mourinho kuisaidia kupata ushindi wa klabu bingwa, ingawa katika matamshi yake ya awali, ilielekea alikuwa hana imani ya klabu yake kupambana na Chelsea.
Fainali ya klabu bingwa itachezwa siku ya Jumamosi, tarehe 19 Mei.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII