HABARI MPYA LEO  

Zitto Vs Chadema urais 2015

By Maganga Media - Mar 26, 2012


SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015, kauli hiyo imewachanganya watendaji wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa. Wakati Dk Slaa akikosoa hatua hiyo na kusema sio wakati mwafaka sasa kuzungumzia urais, Mbowe amesema hana tatizo na Zitto kutangaza nia hiyo sasa kwa kuwa ni haki yake, lakini akahoji haraka ya kutangaza dhamira hiyo.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi hao wamemshauri Zitto kufuata taratibu za chama kama anataka kufikia malengo yake hayo ya kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.

Kauli ya Dk Slaa
Akizungumzia uamuzi huo wa Zitto kutangaza dhamira hiyo, Dk Slaa alisema suala la urais sio muhimu kwa sasa kwani chama kinaangalia ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki. "Naomba niseme hivi, sasa urais sio ‘issue’ (suala). Chama kinaangalia uchaguzi wa Arumeru Mashariki, muda wa kuzungumzia urais ukifika, tutasema," alisema Dk slaa na kuongeza:

“…Naomba mtambue kwamba tunakabiliwa na suala kubwa la uchaguzi huku Arumeru kwa hiyo sasa siwezi kuzungumzia suala la urais, hili sio wakati wake sasa.”

Hata hivyo alimshauri Zitto kufuata taratibu kama ana nia ya kugombea urais na kufafanua kwamba, chama kina utaratibu wake na ndicho chenye uamuzi wa mwisho. “Chadema ina utaratibu wake kwa kila jambo, kama Zitto ametangaza kugombea urais 2015 huo ni uamuzi wake binafsi. Lakini mimi kama kiongozi wa chama sioni kama urais ni jambo la  kujadili wakati huu. “Ikifika wakati wakujadili masuala ya urais, tutafanya hivyo kwa undani lakini, sio kwa sasa kwani wakati wake haujafika.” 

Mbowe
Kwa upande wake Mwenyekiti Mbowe, alisema kila mtu ana busara na haki zake katika kuamua jambo na hii, ni busara yake Zitto. Lakini, Mbowe alionyesha kushangazwa na  Zitto kutangaza nia hiyo sasa wakati ambao chama kinawaza na kufikiria uchaguzi wa Arumeru Mashariki. Mbowe alisema haoni tatizo Zitto kutangaza sasa nia ya kuutaka urais kwa kuwa ni uamuzi na haki yake kwasababu kila mwanachama wa Chadema ana haki ya kuamua jambo analolitaka ili mradi afuate taratibu.

“Sioni kama Zitto ana tatizo lolote la kutangaza sasa kwamba mwaka 2015 anataka kugombea urais kwani ni haki ya kila mtu kugombea nafasi hiyo,” alisema Mbowe. Hata hivyo, alifafanua kwamba pamoja na Zitto kutangaza nia, wakati wa kuwania nafasi hiyo ndani ya chama ukifika wanachama wa Chadema ndio watakaotoa uamuzi wa nani anafaa.

Kauli ya Zitto
Jana, Zitto alipotakiwa kuzungumzia maoni ya Dk Slaa na Mbowe kuhusu uamuzi wake huo, alisema aliamua kutoa taarifa hiyo, kuondoa upotoshwaji ulikuwa ukifanywa na baadhi ya watu baada ya mjadala wake na January Makamba kuhusu umri wa Urais.

Alifafanua kuwa pamoja na kwamba ana nia ya kugombea urais, kwa sasa Chadema inachofikiria ni ushindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki. "Naomba niseme kuwa pamoja na kutangaza nia hiyo, hivi sasa 'focus'(mlengo) yetu ni uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kwa kuwa lazima tulichukue jimbo," alisema Zitto.

Juzi, Zitto alituma taarifa rasmi kwenye gazeti hili akieleza nia yake ya kutaka kugombea urais mwaka 2015. “Kwanza niseme wazi kabisa kuwa urais ninautaka, nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi.”

Alitamba anao uwezo kwa kuwa ni mzalendo, mwenye utashi wa kuleta mabadiliko stahiki kulingana na nchi inavyoongozwa. Alisema mabadiliko makubwa yanahitaji  maamuzi magumu yatakayoudhi wengi hasa vigogo wa nchi za Magharibi huku akitoa mfano kuwa ni pamoja na kuzuia nchi kuuza malighafi pekee.

Alisisitiza kuwa rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo ya nchi na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi. Zitto alisema, mjadala wa umri wa kugombea urais aliouanzisha na Makamba ni mkali na kwamba baadhi ya watu kwa sababu zao binafsi, wameamua kuuita ni mjadala wake na mbunge huyo wa  Bumbuli unaowabagua wazee. 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII