HABARI MPYA LEO  

UDOM KUFUNDISHA KWA MTANDAO

By Maganga Media - Mar 30, 2012

CHSS
MFUMO wa ufundishaji kwa kutumia Mtandao wa Teknohama, umeingia rasmi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kwa sasa, uongozi wa chuo umeanza mchakato wa kuhakikisha kuwa kila mhadhiri, anafundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja. Hayo yalisemwa juzi na Balozi Juma Mwapachu, alipokuwa akizungumza na wahadhiri wa Udom katika ufunguzi wa mafunzo ya ufundishaji kwa njia ya teknolojia hiyo.

Balozi Mwapachu ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, alisema dunia ya sasa ni ya sayansi na teknolojia na kwamba vyuo vikubwa kama Udom, lazima vibadili mitaala yake na kufundisha kwa njia ya kisasa. “Chuo hiki kimebaini kuwepo kwa changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutokuwa na uwiano wa kuridhisha katiya  walimu na wanafunzi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na changamoto hizi azima zifanyiwe kazi ili zisiathiri utoaji wa taaluma,’’alisema Balozi Mwapachu.

Alisema wingi wa wanafunzi katika chuo hicho kikubwa kwa sasa hauendani na idadi ya wahadhiri waliopo na kwamba bila ya  kuwa na mbinu mbadala za kuwafundisha, wanafunzi wataachwa nyuma.  “Udom siyo chuo cha kawaida katika nchi za Afrika Mashariki, lakini pia niseme kuwa siyo vyuo vingi hapa duniani vimeweza kupata bahati ya kukua kwa kasi kubwa ndani ya miaka minne kama Udom, kwa hiyo ukuaji wa chuo hiki lazima uwe wa kisasa na unaokwenda na sayansi na teknolijia,” alisema

Balozi Mwapachu pia aliitaka Serikali kuongeza nguvu katika kukisaidia chuo hasa wa kukipatia  vitendea kazi na miundombinu bora.Kwa mujibu wa Balozi Mwapachu, mfumo wa Teknohama unawezesha pia hata wahadhiri kutoka nje ya nchi, kufundisha wakiwa katika nchi zao.Kuhusu miundombinu ya  maji, umeme na barabara, alisema  lazima iangaliwe vizuri na kutengewa bajeti ya kutosha.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Udom, Prof Idris Kikula, alisema chuo kilikuwa kinakabiliwa na tatizo katika ufundishaji, hatua iliyoulazimisha uongozi kubuni mkakati huo.Kikula alisema hatua ya sasa ni ya kuwajengea uwezo wahadhiri, ili waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII